STAMICO ndani ya maelekezo mazito kuokoa maisha

KATIKA hatua kubwa ya kimkakati inayolenga kuchochea uchumi wa viwanda na kulinda ikolojia ya nchi, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuongeza kasi ya uzalishaji wa nishati safi ili kuokoa maisha ya Watanzania na kukomesha kasi ya ukataji miti kiholela.

Waziri Mavunde ametoa agizo hilo leo, Februari 21, 2026, wakati akizindua kiwanda cha mkaa mbadala cha Rafiki Briquettes kilichopo Kata ya Kiloleni, Manispaa ya Tabora.

Uzinduzi wa kiwanda hicho unatajwa kuwa ni mkombozi wa mazingira kwani unatumia mkaa wa mawe uliochenjuliwa, ambao ni suluhisho la kudumu kwa taasisi na matumizi ya majumbani badala ya mkaa wa miti.

Akizungumzia ustawi wa jamii na afya ya binadamu, Waziri Mavunde ameanika takwimu za kutisha zinazoonesha kuwa takriban watu milioni nne duniani kote hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa yanayosababishwa na nishati chafu kama kuni na mkaa. Alisisitiza kuwa mkaa huu mbadala si tu unalinda mapafu ya mama lishe na wapishi, bali pia ni kinga dhidi ya vifo vinavyoweza kuepukika.

Katika upande wa fursa na ajira, Serikali imewahimiza vijana mkoani Tabora kuchangamkia fursa zinazozalishwa na kiwanda hicho. Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, aliwataka vijana kuacha kulalamika na badala yake kujiingiza katika mnyororo wa thamani wa kiwanda hicho, kuanzia uzalishaji hadi usambazaji wa nishati hiyo safi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amewahakikishia wananchi kuwa suala la uhaba wa nishati sasa ni historia. Alibainisha kuwa kiwanda hicho kina uwezo mkubwa wa kuzalisha tani 20 za mkaa mbadala kwa saa moja, hali itakayohakikisha soko linapata nishati hiyo kwa gharama nafuu na kwa wakati wote bila kuathiri misitu ya nchi.

Kiwanda hiki cha Rafiki Briquettes kinatajwa kuwa ni alama ya mshikamano kati ya sekta ya madini na utunzaji wa mazingira, kikilenga kuivusha Tanzania kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2034, kama ilivyo azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Chapisha Maoni

0 Maoni