Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za kidini katika kudumisha amani na utulivu nchini.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo alipofungua Ijitimai ya Kimataifa ya kila mwaka inayoandaliwa na Jumuiya ya Fissabilillah Tabligh Markaz, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi pamoja na taasisi za kidini ili kuhakikisha nchi inaendelea kubaki katika hali ya amani na mshikamano.
Ameeleza kuwa Uislamu unasisitiza elimu, mawaidha na hekima katika maisha ya kila siku, huku akibainisha kuwa jukumu la kuamrisha mema si la viongozi wa dini pekee bali ni wajibu wa kila muumini kuhamasishana kutenda mema na kusaidiana.
Aidha, amewahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kuzidisha ibada na kumcha Mwenyezi Mungu, sambamba na kuwataka wafanyabiashara kuacha kupandisha bei za bidhaa za chakula wakati wa Ramadhan.
Mapema, Alhaj Dkt. Mwinyi alijumuika na waumini katika ibada ya Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa katika Msikiti huo.
Ijitimai hiyo ya Kimataifa imehudhuriwa na Masheikh pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati.


.jpeg)
0 Maoni