Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar inahitaji vyuo vikuu zaidi ili kuifanya kuwa kituo kinachotambulika kimataifa katika utoaji wa mafunzo, kukuza diplomasia ya elimu na huduma za kitaaluma.
Ameyasema hayo alipokutana na wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na Spika, Mhe. Mussa Azan Zungu.
Rais Dkt. Mwinyi ameridhishwa na wazo la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Diplomasia na Huduma za Bunge kinachotarajiwa kujengwa Zanzibar, akibainisha kuwa kitachochea ujio wa wanafunzi na wageni kutoka mataifa mbalimbali na kuongeza mapato ya nchi. Ameuhakikishia ujumbe huo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kuliunga mkono wazo hilo na kusisitiza utekelezaji wa haraka.
Awali, Spika Zungu alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa uongozi ulioleta mabadiliko chanya na maendeleo katika miundombinu ya barabara na kasi ya ukuaji wa uchumi.
Baada ya mkutano huo, Rais Dkt. Mwinyi amekutana na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, aliyeambatana na watendaji wakuu wa Wizara hiyo kwa ajili ya kujitambulisha.
Dkt. Mwinyi amesema ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wizara ya Fedha unasaidia kutoa ufumbuzi wa haraka kwa changamoto za masuala ya Muungano, akisisitiza umuhimu wa utaratibu bora zaidi katika upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa. Waziri huyo amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi ushirikiano wa hali ya juu katika kuimarisha fursa za kifedha na kiuchumi kwa manufaa ya pande zote za Muungano.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amekutana na Mwakilishi wa Kidiplomasia wa Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan Kanda ya Afrika Mashariki, Ndg. Amin Mawji, akiambatana na Mratibu wa AKDN Zanzibar, Ndg. Rahim Bhaloo. Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano, huku Rais Dkt. Mwinyi akiupongeza mfuko huo kwa mchango wake katika sekta za afya, elimu na mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji.



0 Maoni