Kundi la vijana 335 kutoka Wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza, ambao awali walikuwa wakiishi katika mazingira magumu na hatarishi mitaani, sasa wameanza ukurasa mpya wa maisha.
Hii ni baada ya kuhitimu mafunzo ya fani mbalimbali katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na kukabidhiwa zana za kazi, hatua wanayokiri kuwa ndiyo mkombozi wa kudumu utakaowaondoa mitaani na kuwafanya wawajibike.
Vijana hao, ambao walitambuliwa kupitia jamii kutokana na kukosa mwelekeo wa kimaisha, wamepatiwa mafunzo hayo kupitia Mradi wa Vema unaotekelezwa na Plan International.
Akizungumza katika hafla ya mahafali yao na kukabidhi vifaa, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, amewataka vijana hao kutumia ujuzi na vifaa walivyopata kama mtaji wa kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
"Serikali imewekeza kwenu ili muweze kujitegemea. Tumieni vifaa hivi kuanzisha karakana zenu na kuendeleza shughuli zenu. Zaidi ya hapo, milango ya mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri iko wazi kwa ajili yenu ili muweze kukuza mitaji yenu," alisema DC Mkalipa.
Mmoja wa wahitimu hao, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alielezea safari yake kutoka mitaani hadi kuwa fundi mwenye ujuzi. Alikiri kuwa mafunzo hayo ni fursa adhimu ambayo imebadilisha fikra zake na kumwepusha na vishawishi vya makundi yasiyofaa.
"Nikiangalia hali yangu ya awali, nikiwa mtu wa kukaa mitaani bila matumaini, lakini serikali na wadau wametusaidia sana. Mafunzo haya yametutoa kwenye hatari ya mitaani na sasa nimeanza uzalishaji. Tayari nimepiga hatua kubwa na vifaa hivi vya ufundi magari na useremala tulivyopewa vinaenda kubadilisha maisha yetu kabisa," alisema mhitimu huyo.
Mkakati wa kuwakwamua vijana hawa ulihusisha kuwaunganisha katika makundi ya hisa (kuweka na kukopa) ili kuwajengea nidhamu ya kifedha. Mpaka sasa, kuna zaidi ya vikundi 53 vyenye wanachama zaidi ya 1,200.
Wahitimu hawa 335 ni sehemu ya kundi la kwanza la watu 400 waliohitimisha mafunzo ya vitendo na kukabidhiwa vifaa vya kazi kulingana na fani zao, ikiwemo ufundi magari na ufundi wa jumla.
DC Mkalipa alisisitiza kuwa msaada huo hautashia kwenye kukabidhi vifaa pekee. Alibainisha kuwa ofisi yake itafanya ufuatiliaji wa karibu kwa kila kijana aliyepata vifaa ili kuhakikisha havijauzwa wala kutelekezwa, bali vinatumika kuzalisha mali na kuajiri vijana wengine waliobakia mitaani.

0 Maoni