Sasa hivi siyo enzi ya kulalamika mtaani, ni enzi ya kuchamkia fursa na kuthubutu kupenya popote pale penye mchongo wa hela. Serikali imekunja shati na kuamua kuingia mkataba wa kibabe na Baraza la Dhahabu Duniani ili kurusha Satelaiti itakayotufungulia ramani ya utajiri uliolala chini ya ardhi.
Huu sio mchongo wa kufanya kwa shinikizo tena, bali ni biashara kamili ambapo David Tait na Profesa Kitila Mkumbo wamekaa mezani na kukubaliana kuwa sasa ni wakati wa teknolojia kufanya kazi yake.
Hapa ndipo kijana mjanja anapopaswa kufumbua macho, maana hii satelaiti haitakuja na wataalamu kutoka nje pekee, bali ni nafasi ya wazawa kuanza kupiga hatua kwenye sayansi ya madini na biashara ya kimataifa bila uoga.
Kama hiyo haitoshi, Mama Sarah Masasi wa Geita Gold Refinery ameweka wazi kuwa uwezo tunao na sababu tunayo, akisisitiza kuwa vijana wa nyumbani wana akili na nguvu ya kupiga kazi yenye viwango vya kimataifa.
Fikiria kampuni ya kizalendo inayoweza kusafisha kilo mia sita za dhahabu kwa siku, hapo ndipo unapoona kuwa kuthubutu ndiyo siri ya kutoboa.
Waziri Anthony Mavunde naye ameshusha nondo kuwa mchango wa vijana na wachimbaji wadogo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi kwa sasa, huku mawaziri wengine kama Joel Nanauka na Dkt. Doroth Gwajima wakihakikisha kuwa kila kijana, awe wa kike au kiume, anapata nafasi yake kwenye huu mnyororo wa thamani.
Ujumbe ni mmoja tu kwa vijana wote wapambanaji: amani tuliyonayo ndiyo mtaji wetu mkuu wa kufanya haya mambo makubwa. Huwezi kurusha satelaiti wala kusafisha dhahabu kishabiki kama nchi haina utulivu, hivyo tuulinde huu umoja wetu ili kesho na keshokutwa tuwe sisi ndio wamiliki wa hizi kampuni kubwa.
Kama wakazi wa Morogoro na Simiyu walivyopiga yowe ya kulinda amani, basi na sisi vijana tutumie amani hiyo kuthubutu kuingia kwenye biashara, teknolojia, na uongozi.
Huu ni wakati wa kuacha kukaa pembeni na kuanza kuwa sehemu ya simulizi ya utajiri wa taifa letu, maana fursa zimefunguka na nchi inawategemea nyinyi wazalendo wenye kiu ya mafanikio.

0 Maoni