Uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa, kama alivyotangaza katika hotuba yake ya kuukaribisha mwaka 2026, ni hatua ya kimkakati inayolenga kuiponya nchi kutokana na majeraha ya kisiasa na kijamii.
Katika
kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika mzunguko mwingine wa kisiasa,
maridhiano si chaguo bali ni hitaji la lazima ili kuhakikisha taifa linabaki kuwa
kitu kimoja. Maana ya hatua hii kwa mwaka 2026 ni kuweka msingi wa kuaminiana
kati ya serikali, vyama vya siasa, na wananchi, ili tofauti za kiitikadi zisiwe
chanzo cha mpasuko bali ziwe chachu ya ujenzi wa demokrasia iliyokomaa.
Pamoja
na kauli hiyo ya upole bado kuna baadhi ya watu
katika mitandao waliendelea kutoa maoni ya dhihaka, matusi ya nguoni, na
lugha za kashfa ikiwa ni kielelezo cha mmomonyoko wa maadili na ukosefu wa
staha ambao unahatarisha jitihada hizi za kuwa na taifa lenye utulivu na amani.
Ni
jambo la kusikitisha kuona kuwa badala ya kujadili muundo na majukumu ya tume
hiyo kwa hoja, baadhi ya watu wanatumia uhuru wa maoni kupandikiza mbegu za
chuki na utengano. Hali hii inathibitisha kuwa ukombozi wa fikra unahitajika
kwa haraka ili jamii itambue kuwa matusi si suluhu ya changamoto za kisiasa.
Kwa
upande mwingine, sauti za busara zinazowahimiza vijana kulinda amani na kutumia
mazungumzo badala ya vurugu ndizo zinazopaswa kupewa kipaumbele.
Tukio
la tarehe 29 Oktoba linapaswa kubaki kama funzo la kudumu kuwa amani
ikishapotea, gharama ya kuirejesha ni kubwa mno. Maridhiano ya kweli hayawezi
kufikiwa ikiwa upande mmoja unatoa mkono wa heri huku upande mwingine ukiwa
umejaza matusi na kashfa viganjani. Ni lazima vijana watambue kuwa wao ndio
walinzi wa urithi wa Tanzania, na kutumiwa kama vyombo vya kuchochea taharuki
ni kujihujumu wenyewe na vizazi vijavyo.
Jukumu
la viongozi wa dini na taasisi za kijamii katika kipindi hiki ni kuwa daraja la
kweli la upatanisho. Tunahitaji sauti zinazounganisha raia na viongozi wao, si
kuta zinazowatenganisha.
Mwaka
2026 unapaswa kuwa mwaka wa ukomavu, ambapo maridhiano yanatazamwa kama fursa
ya kurekebisha makosa ya nyuma na kuimarisha mshikamano.
Tanzania
ni nyumba yetu sote, na ujenzi wa nyumba hii unategemea utulivu, heshima kwa
mamlaka, na uwezo wetu wa kukaa meza moja na kukubaliana kutokubaliana bila
kutukanana. Huu ndio wakati wa kuweka nchi kwanza na kuacha siasa za chuki
ambazo hazina tija kwa maendeleo ya taifa letu.

0 Maoni