Jeshi la Polisi Tanzania limetoa wito
kwa umma kuendelea kudumisha amani na utulivu, huku likisisitiza kuwa
linashuhudia juhudi za mara kwa mara za kubadilisha mbinu za uchochezi zenye
lengo la kuingiza vurugu na chuki nchini.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa
Jeshi la Polisi, Makao Makuu, mjini Dodoma, David Misime imesisitiza umuhimu wa
kushirikiana na kukataa uchochezi huo.
“Tukatae yale yote yanayohamasishwa
kwa njia mbalimbali na katika maneno ya kubadilisha mbinu kila mara ili kutaka
kutuchonganisha na kutujengea chuki kati yetu.”
Taarifa hiyo iliongeza kuwa lengo la
vitendo hivyo vya uchochezi ni “kutuuingiza katika vurugu ambazo matokeo yake
siyo mazuri kama tunavyo shuhudia katika maeneo mengine duniani.”
Hali ya Usalama Nchini Iko Shwari
Wito huo wa Polisi unakuja siku moja
baada ya kutoa taarifa ya kuhakikisha Watanzania hali ya usalama. Jeshi la
Polisi, kupitia taarifa yake, limewajulisha wananchi kuwa, “kwa ushirikiano wa
Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na ninyi wananchi na wadau wengine katika
kutimiza jukumu la kulinda amani, utulivu na usalama nchini, hadi sasa nchi
yetu kiusalama ni shwari na shughuli za kiuchumi na za kijamii ziliendelea
vizuri katika mazingira ya amani kwa kipindi hicho cha masaa 24.”
Jeshi hilo limeeleza kuwa
wanapoendelea kuelekea siku ya mwisho wa wiki, wanatoa wito kwa kila mmoja
kuendelea kutii sheria, kushirikiana na kila mmoja na kutekeleza wajibu wake
katika kulinda na kuimarisha amani ambayo kila mmoja anaihitaji katika maisha
na shughuli zake za kila siku.
Jeshi la Polisi limeahidi kuwa, kwa
kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, litaendelea kulinda
usalama wa nchi yote, maisha na mali za kila mmoja, pamoja na Taifa
zima la Tanzania.

0 Maoni