WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa maagizo kwa viongozi wa majiji na halmashauri zote nchini kuhakikisha wafanyabiashara hawanyang’anywi bidhaa zao na badala yake wawaelekeze namna bora ya kufuata taratibu zilizowekwa.
“…Msichukue bidhaa za raia; hizo ndio ofisi za raia
wetu, hata kama kuna jambo ambalo anapaswa kuelekezwa kuhusu masuala ya
utaratibu basi mshughulikie jambo linalohusu utaratibu, msizuie mitaji ya watu.
Utaratibu wa kuchukua bidhaa haukubaliki na hakuna uhalali wa kuchukua bidhaa
za raia. Msicheze na mitaji ya watu.”
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu,
Desemba 8, 2025) wakati akizungumza na wafanyabiashara katika soko la Machinga
jijini Dodoma baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Richard Joseph ambaye ni
mfanyabiashara sokoni hapo aliyedai kuchukuliwa bidhaa zake na watumishi wa
jiji.
Mheshimiwa Dkt Mwigulu amemuagiza mkuu wa mkoa wa
Dodoma Rosemary Senyamule pamoja na Mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri
wahakikishe wanafuatilia suala hilo na wahusika warudishe bidhaa za
mfanyabiashara. “Kama wamepotea nazo, wachukuliwe hatua kama wezi
wengine. Mheshimiwa Rais hapendi uonevu, ni mtu wa haki.”
Waziri Mkuu ambaye amefanya ziara ya kushtukiza
sokoni hapo ameagiza wafanyabiashara kutoondolewa kwenye vizimba vyao na kama
bado kuna mahitaji makubwa ya maeneo ya kufanyia biashara uongozi wa mkoa
utafute maeneo na kujenga masoko ili kutosheleza mahitaji.
Kwa upande wao wafanyabiashara katika soko hilo
wamemshukuru Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa kufanya ziara hiyo ya kushtukiza na
kusikiliza kero zao na kumuomba aendeleze utaratibu huo na maeneo mengine ya
nchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amewasisitiza
Watanzania kuendelea kudumisha amani na mshikamano ili waweze kufikia malengo
ya kimaendeleo yaliyowekwa na Serikali. “Watanzania tukatae kugawanywa.”
Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya siku ya Uhuru,
Waziri Mkuu amewasihi wananchi kuitumia siku hiyo kwa ajili ya mapumziko
isipokuwa kwa wale ambao watalazimika kwenda kazini kutokana
na majukumu yao.


0 Maoni