WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema ni lazima
yafanyike mapitio ya haraka kwenye tamko la mali na madeni na yawe na madaraja
kwa sababu kuna maeneo ambayo bado rushwa imekithiri lakini watumishi wake
hawajajumuishwa kwenye mfumo kama viongozi wa umma.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Desemba
11, 2025), alipozungumza na Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, alipotembelea ofisi hizo zilizopo Mtaa wa Tambuka
Reli, Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuiagiza
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhakikisha uadilifu unasimamiwa
kuanzia katika sheria, kanuni na utekelezaji ili rasilimali za Taifa ziweze
kuwanufaisha wananchi wote.
Amesema kuwa yapo maeneo ambayo fedha za umma huwa
zinapotea hivyo yawekewe uangalizi wa kutosha. “Bado kuna kazi kubwa katika
usimamizi wa maadili ya umma, suala hili Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan amelisisitizia sana”
Ameiagiza taasisi hiyo ishirikiane na taasisi
nyingine ikiwemo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuhakikisha
wanaziba mianya yote ya rushwa kwa kuchunguza matamko yanayowasilishwa na
viongozi kama yamejazwa kwa usahihi.
“…Bainisheni maeneo yenye rekodi za rushwa na yapewe
kipaumbele; fomu zijazwe kuendana na uhalisia wa taarifa za mhusika. Lazima
kila mtu aogope mali ya umma, msipochunguza, wananchi watachunguza wenyewe.”
Mheshimiwa Waziri Mkuu ametolea mfano maeneo ambayo
yanatuhumiwa kuwa na mianya ya rushwa ni pamoja na michakato ya manunuzi,
utiaji saini wa mikataba mbalimbali na maeneo ya makusanyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ina kazi kubwa ya kuhakikisha nchi
inaendeshwa kimaadili.



0 Maoni