Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mbinga imepokea jumla ya shilingi milioni
403,772,750.00 kutoka serikali kuu kwa ajili ya kurejesha mawasiliano ya
barabara zilizoharibiwa na mvua za masika pamoja na tetemeko la ardhi
lililotokea mwezi Mei, 2024.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga, Mhandisi Oscar Mussa,
amesema kuwa fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi miwili mikubwa ya
ukarabati wa barabara ambazo zilikuwa muhimu kwa wakazi wa maeneo husika.
"Katika kipindi cha masika tulikumbwa na madhira
makubwa yaliyosababisha kuporomoka kwa udongo na kuharibu miundombinu ya
barabara. Serikali ilitupatia shilingi milioni 283,172,000.00 kwa ajili ya
kurudisha mawasiliano katika barabara ya Langilo kuelekea mkoha," amesema
Mhandisi Musa.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 7.2 inahudumia wakazi
wa Kata ya Langilo, hususan kijiji cha Mkoha. Madhara makubwa yalitokea katika
eneo la daraja la mto Makomba ambapo udongo uliporomoka na maeneo mengine
yaliathiriwa na mawe yaliyoporomoka kwenye kona za barabara hiyo.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza mwezi Machi mwaka
huu na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba na kuongeza kuwa kazi
zilizokamilika hadi sasa ni pamoja na kurudisha tuta, kujenga mitaro ya maji ya
mvua yenye urefu wa zaidi ya Km 1 na kuondoa mawe yaliyokuwa yameziba barabara.
Ametaja mradi wa pili ni ukarabati wa barabara ya
Longa–Kipololo–Litoho, ambayo imepokea shilingi milioni 120,600,750.00 baada ya
kuathiriwa na tetemeko la ardhi. “Eneo la Kalavati la mto Ntunduwalo, hususani
katika barabara ya Longa liliporomoka tuta, lakini kwa sasa barabara hiyo
imefunguliwa na inapitika kwa usalama”.
Mhandisi Mussa ameishukuru serikali kwa kuwezesha kupata
fedha hizo kwani wananchi wa Mbinga wanaendelea kutoa shukrani kwa uwezeshaji
huu ambao umeleta nafuu katika usafiri na usafirishaji pamoja na uchumi wa
maeneo husika,


0 Maoni