Siku chache
baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, kuzindua Makumbusho
ya kisasa ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai (Urithi Geo Museum) tarehe 16 Oktoba,
2025 wadau wameanza kuvutiwa na makumbusho hiyo na kuitembelea kwa lengo la
kupata elimu kuhusu vivutio vya utalii, shughuli za uhifadhi wa maliasili na
mambo kale.
Watalii na
wadau wanaotembelea jengo hilo wanapata elimu kuhusu muonekano wa dunia miaka
milioni mia mbili iliyopita na ilivyo sasa, maumbile asilia yanayopatikana
katika ukanda wa bonde la ufa,kujionea mwamba wenye umri wa miaka milioni tatu
iliyopita unaopatikana hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro-Lengai, kujifunza
tamaduni za makabila ya Wahadzabe,
Wairaqw, Wadatoga na Wamasai pamoja, kupima uwezo wa kutambua sauti za
wanyamapori, kushindana mbio kwa kutumia baiskeli na wanyamapori ndani ya maakumbusho na ameengine mengi.
Miongoni
wadau waliotembelea Makumbusho hiyo ni kundi la wanakwaya 22 wa KKKT Dayosisi
ya kasikazini Jimbo la karatu usharika wa Qurus ambapo wametembelea jengo la Makumbusho kwa lengo la
kujifunza vitu vilivyopo na kurekodi wimbo wa kwaya kwa ajili ya albam yao
inayoitwa "Tumetoka mbali"
Kiongozi wa
Kwaya hiyo Mwinjilisti Eliamani Kimay ameeleza kuwa kwaya hiyo kuamua kurekodi
wimbo katika maeneo ya makumbusho hiyo ni kutokana na muonekano wa jengo hilo
na maelezo ya vivutio vya utalii vilivyopo ndani ambapo kupitia kwaya hiyo
wanatangaza injili kwa kutumia jengo hilo ambalo ndani yake kuna vioneshwa vya
kipekee vinavyoashiria uumbaji wa mungu.
Mmoja wa
wanakwaya wa kundi hilo Bi. Mariam Emmanuel ameeleza kuwa uamuzi wa kwaya yao
kurekodi katika jengo hilo ni kuonesha
vivutio vilivyopo Ngorongoro, kutangaza jengo hilo kupitia injili, kuonesha
vivutio vilivyopo ndani ya makumbusho ili kuhamasisha wananchi wengi zaidi
kupata elimu juu ya uumbaji wa mungu, kufahamu masuala ya kijiolojia, urithi wa
utamadani, malikale, historia ya chimbuko la binadamu ambayo kwa pamoja
yanaashiria uumbaji wa mungu.
Eneo la
Hifadhi ya Ngorongoro ilipewa hadhi ya kuwa eneo lenye utalii wa Miamba
“Geopark” mwaka 2018 na kuwa Jiopaki
pekee katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara na ya pili kwa Afrika ikitanguliwa na Morocco.




0 Maoni