Chama cha Mawakili wa Serikali kinatoa pongezi za dhati kwa
Mheshimiwa Hamza Saidi Johari kwa kuteuliwa tena kuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali. Uteuzi huu unaakisi ubobezi na uadilifu wake katika taaluma ya
sheria, sambamba na matakwa ya Ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inayotaka Mwanasheria Mkuu awe na sifa za uwakili kwa angalau miaka
kumi na tano.
Mhe. Johari ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika utumishi
wa umma, hasa katika masuala ya mikataba, sheria za anga, bahari na udhibiti.
Ana Shahada ya Sheria (LL.B) na Shahada ya Uzamili (LL.M) katika Sheria za
Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Kiev, Ukraine, pamoja na cheti cha Uongozi na
Usimamizi kutoka Chuo cha Utawala cha India.
Amehudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga
Tanzania kwa miaka tisa na amewahi kuwa Mwenyekiti wa CANSO Afrika, CASSOA, na
Kamati mbalimbali za kisheria za kikanda na kimataifa. Aidha, amewahi
kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mzumbe na Alexandria (Misri).
Mhe. Johari amekuwa Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali,
Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, na Mwenyekiti wa Timu za Majadiliano ya
Serikali katika mikataba mikubwa ya kimataifa ikiwemo DP World (U.A.E) na
Bandari ya Adani (India). Pia ameshiriki katika timu za kitaifa za kutatua
migogoro ya mipaka na majadiliano ya miradi ya kimkakati ya nchi.
Mhe. Johari ni Mmakonde mzaliwa wa wilaya ya Mtwara
Vijijini, Tarafa ya Ziwani kata ya Nalingu.
Kwa mchango wake mkubwa katika kukuza taaluma ya sheria,
uongozi bora na uzalendo, Chama cha Mawakili wa Serikali kinampongeza kwa dhati
na kumtakia mafanikio zaidi katika majukumu yake mapya.
Imetolewa na: CHAMA CHA MAWAKILI WA SERIKALI TANZANIA

0 Maoni