Kamishna wa
Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Bw. Abdul-Razaq Badru
ameeleza kuwa kusimamia na kuendeleza uhifadhi ni jukumu la msingi kwa mamlaka
hiyo kwani uhifadhi ndiyo moyo katika ustawi wa utalii na
maendeleo ya jamii.
Akizungumza
na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika ofisi za makao makuu Karatu
Arusha leo tarehe 7 Novermba, 2025 Kamishna Badru amesisitiza kuwa, usimamizi
madhubuti wa rasilimali za wanyamapori, Misitu na Malikale zilizopo hifadhi ya
Ngorongoro ni jambo la kufa na kupona na kueleza watumishi hao kuwahudumia
wageni wanaotembelea hifadhi kwa wakati, ukarimu, uadilifu na nidhamu ili
kuendelea kulinda chapa ya Ngorongoro (Brand) kama eneo bora la utalii wa
kifahari (Premium Safari Destination).
“Jukumu la
msingi kwa kila mtumishi wa Ngorongoro ni Uhifadhi kisha mengine yanafuata, uhifadhi
na ulinzi wa rasilimali ni jambo la kufa na kupona, hivyo nawasisitiza kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa
rasilimali hizo.
Akitoa
taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo Naibu Kamishna anayeshughulikia
uhifadhi,utalii na maendeleo ya jamii Joas Makwati ameeleza kuwa idadi ya
watalii imeendelea kuongezeka ambapo robo ya kwanza iliyoishia Septemba 2025
zaidi ya watalii 350,000 wametembelea Ngorongoro.
Kwa upande
wake Naibu Kamishna anayeshughulikia huduma za shirika Aidan Makalla amewataka
watumishi kuwa wazi kuchangia maendeleo ya mamlaka kwa kuendelea kutoa ushauri,
maoni na Mtazamo katika majukumu ya taasisi ili kuhakikisha huduma zinaendelea
kuwa bora na endelevu.
Na Mwandishi wa NCAA- Karatu.




0 Maoni