KESHO ni siku rasmi ya Uchaguzi Mkuu, tukio muhimu
la kidemokrasia linalowakutanisha Watanzania katika vituo vya kupigia kura kote
nchini. Katika hali ya msisimko wa kisiasa unaoshuhudiwa tangu kuanza kwa
kampeni hadi hitimisho lake, wito mkuu unaotolewa na wadau wote wa siasa,
ikiwemo vyama vikuu vya upinzani kama ACT-Wazalendo na CUF, ni mmoja:
Watanzania wafanye uamuzi wao kwa Amani na Busara.
Wito huu unakuja kuwakumbusha kila mmoja aliye na
Kitambulisho cha Mpiga Kura kwamba uhai wa Taifa unategemea jinsi gani tunasimamia
haki yetu ya Kikatiba. Amani na utulivu uliojengwa kwa miongo mingi haupaswi
kuharibiwa na mazingira ya ushindani wa kisiasa.
Kwa mujibu wa misimamo ya viongozi wa upinzani,
amani inakwenda sambamba na haki. Kauli za ACT-Wazalendo zimekuwa zikisisitiza
kuwa amani ya kweli inapatikana pale haki na utawala wa sheria unapozingatiwa
katika kila hatua ya mchakato. Kwa chama hicho, kushiriki kwa utulivu
kunamaanisha kila mwananchi anapaswa kutii sheria za uchaguzi, kuepuka vitendo
vya uchochezi au vurugu, na pia kuwa tayari kuvumiliana na kukabiliana na
changamoto zozote zinazoweza kutokea kwa utulivu, wakijua kuwa Tanzania ni ya
kwanza na ya mwisho.
CUF pia imeunga mkono wito wa kitaifa unaohimiza
uchaguzi ufanyike kwa huru, haki na amani. Chama hicho kinawahimiza Watanzania
kujitokeza kwa wingi bila hofu na kuitumia haki yao ya kupiga kura kwa umakini,
huku wakisisitiza kwamba uchaguzi wao unajengwa juu ya matumaini ya mchakato
safi na wa amani.
Utaratibu Rahisi wa Kupiga Kura 
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imekuwa
inawakumbusha wapiga kura kufuata utaratibu sahihi wa upigaji kura hapo kesho.
Kwanza kabisa, mwananchi anatakiwa kufika Kituoni kwake na kuonyesha
Kitambulisho chake cha Mpiga Kura ili Afisa wa Tume athibitishe jina lake
katika Daftari. Baada ya uthibitisho huo, mpiga kura atapewa karatasi tatu za
kupigia kura: moja kwa Urais, ya pili kwa Ubunge na ya tatu kwa Udiwani.
Akiwa amechukua karatasi hizo, mwananchi anatakiwa
kuingia katika chumba cha siri ambapo ataweka alama ya 'vema' au 'X' kwa
mgombea anayemtaka kwenye kila karatasi. Ni muhimu sana kuhakikisha hauweki
alama zaidi ya moja wala kutoa siri ya kura yake kwa mtu mwingine yeyote. Baada
ya kumaliza kupiga kura kwa siri, mpiga kura atatoka chumbani na kutumbukiza
kila karatasi katika Sanduku la Kura linalostahili kabla ya kuondoka Kituoni
kwa utulivu, kutoa nafasi kwa wapiga kura wengine kuendelea.

0 Maoni