Zoezi la uthamini maeneo yatakayopitiwa na ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa SGR kipande cha 6 kutoka Tabora hadi Kigoma linaendelea kwa kasi katika wilaya sita za mikoa hiyo.
Wilaya hizo ni Tabora
Mjini, Uyui, Urambo, Kaliua, Uvinza pamoja na wilaya ya Kigoma. 
Timu kutoka ofisi ya
Mthamini Mkuu wa Serikali ikiongozwa na Mthamini Kiongozi FRV James Mark
Mwanakatwe ipo mkoani kigoma ikiendelea na kazi ya uhamasishaji pamoja na
ukusanyaji taarifa za mali uwandani kwa wananchi ambao maeneo yao yanaguswa  na mradi huo.
Akizungumza wakati wa
utoaji elimu na zoezi la uthamini uwandani tarehe 27 Oktoba 2025 wilayani
Kigoma FRV Mwanakatwe ameeleza kuwa, Ofisi ya Mthamini mkuu wa Serikali imepewa
jukumu na serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kufanya uthamini wa
fidia kwa kipande cha 2 hadi 6 ambapo kwa sasa wako kipande cha sita.
Kwa mujibu wa FRV
Mwanakatwe, timu yake imeshafanya uthamini wa vipande 52 (land parcel) ikiwemo
kipande cha daraja la mto Malagarasi lenye urefu km 3 ambalo liko katika hatua
za mwisho za utekelezaji.
Amesema, kwa zoezi
linaloendelea sasa, wanaendelea na uthamini wa 
kilomita 72 hususan kwenye maeneo ambayo ni vipaumbele vya mkandarasi na
kuweka wazi kuwa, kazi hiyo ina takriban vipande 44.
"Kwa kazi hii ni
kilomita 72 na vipande vya ardhi takriban 44 ambavyo tutavifanyia kazi na
tumeanza kazi rasmi hapa" amesema.
Mthamini huyo kiongozi
wa Mradi wa SGR kipande cha 6 ameeleza kuwa, wameshafanya utafiti wa viwango
vya fidia pamoja na kutoa elimu  kwa
wananchi wanaopitiwa na mradi huo   ili
wafahamu na kuzingitia masuala yanayohusu fidia.
Aidha, amebainisha
kuwa, uthamini wa fidia kwa sasa 
unaendelea kwa kasi na timu ya Mthamini Mkuu wa Serikali  itaendelea na jukumu lake la uthamini kwa
umakini na uweledi mkubwa ili kufanikisha kazi hiyo kwa wakati.
Mkazi wa Nyamoli
wilayani Kigoma ambaye eneo lake linapitiwa na mradi wa SGR Bw. Petrick Mathias
amesema, wameupokea mradi huo kwa furaha kubwa na kueleza kuwa, ni imani yao
wanaopitiwa na mradi huo  watalipwa fidia
kwa viwango stahili.
"Tumeupokea mradi
huu kwa mikono miwili na ni matumaini yetu malipo ya fidia yatatolewa kwa
viwango stahili" amesema.
Naye Amina Ashrafu
ameshukuru timu iliyotoa elimu kuhusu masuala ya uthamini wa fidia na kueleza
kuwa, fidia iliyofanyika maeneo mengine ya mradi huo wa SGR yanawapa imani
kuwa, nao watalipwa kwa haki na viwango stahili.
Na. Munir Shemweta- WANMM



0 Maoni