Mgombea Ubunge wa Jimbo
la Bukombe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Doto Mashaka Biteko amewaomba
wananchi wa Jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kumchagua mgombea wa Urais kupitia
CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan ili Chama hicho kiendelee kuongoza na kuliletea
Taifa maendeleo.
Dkt. Biteko ametoa rai
hiyo Oktoba 27, 2025 wakati akihitimisha kampeni za Uchaguzi Mkuu zilizofanyika
katika Uwanja wa Kata ya Igulwa, Bukombe, mkoani Geita ambapo amesema wananchi
wa Bukombe wana kila sababu ya kujitokeza kupiga kura “Kuvemesha” ifikapo
Oktoba 29, 2025.
“ Maendeleo yote katika
jimbo letu na maeneo mengine ya nchi ni kutokana na mapenzi makubwa aliyonayo
Dkt. Samia kwa wananchi wake, hivyo tarehe 29 Oktoba 2025 twendeni tukampe kura
nyingi za heshima na shukrani kwa mapenzi yake kwetu,” amesema Dkt. Biteko.
Pia amewahimiza wananchi
hao wampigie kura za ndiyo Mgombea wa Ubunge Dkt. Biteko pamoja na madiwani wa
CCM ili waendeleze mipango ya maendeleo.
“ Tusibweteke kwa kauli
za kutiki bila kujitokeza kupiga kura kwa viongozi watakaoleta maendeleo. Hivyo
siku ya Jumatano Oktoba 29, tukapige kura nyingi kwa Dkt. Samia, Wabunge na
Madiwani wa CCM na hapo tutakuwa tumetenda haki.” amesisitiza Dkt. Biteko.
Aidha, amewashukuru
wana Bukombe kwa ushirikiano wao kwa kipindi chote cha kampeni na kuahidi
kuendeleza ushirikiano huo kwa kulinda na kufanikisha miradi mbalimbali ya
maendeleo.
"Nataka niwaambie
wana Bukombe huwa mnanipa deni kubwa sana moyoni mwangu hamjui tu, huwa hamjui
huwa najiona mmenipa stahili nisiyostahili kwa sababu kama binadamu nina
mapungufu yangu mengi lakini mnanipa heshima,” amebainisha Dkt. Biteko.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wa Mkoa wa Geita, Nicholous Kasendamila
amehimiza wananchi wa Mkoa huo kutumia haki yao ya Kidemokrasia na kujitokeza
kupiga kura. “ Kazi ya kampeni iliyodumu kwa takribani miezi miwili haitakuwa
na maana endapo hatutajitokeza kupiga kura.”
Kampeni hizo za Urais,
Ubunge na Udiwani kwa Jimbo la Geita zilizinduliwa Septemba 2, 2025 ambapo
Kampeni za kitaifa zitahitimishwa siku ya Jumanne Oktoba 28, 2025 katika Uwanja
wa Kirumba, mkoani Mwanza.



0 Maoni