Kesho ni Siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani, na wakati Watanzania wakiingia vituoni kupiga kura, wito maalum wa
kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa unatolewa na viongozi wa dini
nchini.
Katika Kongamano la Viongozi wa Dini Kanda ya Kati,
lililofanyika jijini Dodoma siku mbili zilizopita, viongozi hao walisisitiza
umuhimu wa wananchi, hasa vijana, kutambua nafasi yao kama nguzo ya Taifa na
kutumia siku ya leo kwa hekima, uwajibikaji na uzalendo.
Akizungumza katika kongamano hilo, Askofu Evance
Chande, wa Kanisa la Carmel Assemblies of God, aliwakumbusha Watanzania kuwa
vijana ndio nguvu ya Taifa, hivyo wana jukumu la kulinda amani na kutumia kura
kama silaha ya maendeleo. Askofu Chande alisisitiza: “Tunapaswa kuikumbatia
amani kama tunavyokumbatia imani zetu. Uchaguzi ukipita, Tanzania inabaki kuwa
moja. Tusikubali kugawanywa kwa misingi ya kisiasa.”
Kaulimbiu ya kongamano hilo ilikuwa, "Kupiga
kura ni haki ya kila Mtanzania, amani na utulivu ni jukumu letu." Sheikh
Mustapha Rajab, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, aliyekuwa mgeni rasmi, aliungana na
wito huo, akisema: “Amani si jambo la bahati mbaya, ni matokeo ya utii,
uvumilivu na kuheshimu mamlaka. Tukitii viongozi wetu wa dini na Serikali,
Taifa litaendelea kubaki salama.”
Wito wa jumla kwa wananchi ni kuendelea kuliombea
Taifa, kuonyesha uvumilivu na maelewano, huku wakisisitiza kwamba amani ni
msingi wa maendeleo, imani, na utajiri mkubwa zaidi wa Tanzania.
Wakati huo huo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
(INEC) imethibitisha utayari wake kamili wa kusimamia uchaguzi wa kesho.
Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, alitoa risala ya
namna ya kufanikisha uchaguzi na akiwa Mkoa wa Katavi kujionea maandalizi ya
ujenzi wa vituo 83 vya kupigia kura vilivyotengwa maalum kwa ajili ya wakazi wa
maeneo yaliyofutwa kiutawala, INEC iko tayari kwa uchaguzi.
Jaji Mwambegele alisema Tume imetoa matangazo katika
maeneo yote yaliyofutwa na imeweka vituo katika maeneo jirani ili kuwawezesha
wapiga kura kushiriki. Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Tanganyika, Bi.
Kagemlo Mutagwaba, alihakikishia kuwa wapiga kura kutoka maeneo hayo
wamehamasishwa na wanaonyesha utayari wa kujitokeza
kupiga kura kesho.

0 Maoni