VIONGOZI wa Dini Wilaya
ya Ikungi mkoani Singida wametoa tamko la kuwaomba wananchi wote wa wilaya hiyo
kushiriki kikamilifu kwa Amani uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho Oktoba 29,
2025.
Tamko hilo wamelitoa
Oktoba 27, 2025 wakati wakizungumza na waandishi habari na kueleza kuwa kila baada ya miaka mitano ifikapo Oktoba nchi hufanya uchaguzi mkuu wa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.
Akizungumza kwa niaba
ya viongozi wa dini wenzake Askofu Philemon Nyika wa Kanisa la International
Evangelism Church Ikungi alisema wakiwa kama walezi wa maadili, amani na
mshikamano katika jamii wanatoa tamko hilo kuhamasisha wananchi wote wa Wilaya
ya Ikungi na Tanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.
“ Kupiga kura ni haki
ya kila mtu kikatiba na ni wajibu wa kizalendo, tunawasihi wananchi wote
waliojiandikisha wajitokeze kwa wingi kesho Oktoba 29, 2025 kwenda kupiga
kura,” alisema Askofu Nyika.
Aidha, Askofu Nyika
aliwataka wananchi kufanya maamuzi ya busara na ya haki kwa kuchagua viongozi
wanaoamini watawatumikia kwa uadilifu huku wakitambua kwamba kura ni haki yao
na kulinda amani ya nchi ni wajibu wa kila mmoja wetu.
Askofu Nyika alisema
kudumisha amani ni msingi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiroho, hivyo
wanawakumbusha wananchi wote kwamba tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo
cha chuki, migawanyiko, maandamano na vurugu siku ya uchaguzi na baada ya
uchaguzi na visipewe nafasi kwa sababu amani ni zawadi kutoka kwa Mungu isichezewe
hata kidogo.
“Sisi Viongozi wa dini
kutoka Wilaya ya Ikungi tutaendelea kuliomba taifa letu liendelee
kuwa na utulivu, mshikamano, upendo na tunawasihi waumini wetu waendelee
kuiombea nchi yetu ya Tanzania,” alisema Askofu Nyika.
Kwa upande wake Sheikh
wa Wilaya ya Ikungi, Abdi Selemani alisema tunapoenda kupiga kura
kesho jambo la kwanza ni kuangalia amani ya nchi yetu kwani amani ni
tamko la lililotoka kwa Mungu na ni jambo kubwa sana.
Tuna wasihi wananchi wa
Wilaya ya Ikungi na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuitunza amani hii tuliyopewa
na Mwenyezi Mungu, alisema Sheikh
Selemani.
Sheikh Selemani
aliwaomba wananchi wote waliojiandikisha kupiga kura kesho Oktoba 29, 2025
kwenda kufanya hivyo kwani ni haki yao na wasipofanya hivyo watakuwa
wamejinyima haki hiyo.
Naye Askofu Jeremia
Samuel wa Kanisa la The Free Pentecostal Church Of Tanzania Jimbo la Ikungi,
alisema kesho Oktoba 29, 2025 ni jukumu la kila Mtanzania aliyejiandikisha
kujitokeza kwenda kupiga kura kwa ajili ya kumchagua Rais wetu, wabunge na
madiwani.
“Kwa bahati nzuri vyama vyote vilivyoshiriki kampeni tumewaona wagombea wao walivyoshiriki kunadi sera za vyama vyao hivyo imetupa urahisi wa kujua ni nani wa kuweza kutuongoza katika taifa letu hivyo ni wito wetu viongozi wa dini kwenu kesho Oktoba 29, 2025 mjitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura,” alisema Askofu Samuel.
Viongozi wa dini
walioshiriki katika mkutano huo ni kutoka Jumuiya Zawwiyyatul Qaadiriyya
Tanzania ambayo,ni muungano wa mazawiyya yote ya Tanzania, Kanisa la
Waadventista Wasabato (SDA), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), The Free
Pentecostal Church Of Tanzania, Kanisa la CPCT na Aswar Suna.

0 Maoni