Jeshi la Polisi limetahadharisha wananchi kuwa,
kuna kikundi cha watu baada ya kuona wameshindwa kuvuruga amani ya nchi
wameunda kikundi cha vijana ambao wanaandaa picha mjongeo na taarifa mbalimbali
za matukio yaliyotokea siku za nyuma ambayo Polisi waliyafanyia kazi na mengine
ya kutunga ili wayasambaze kwenye mitandao ya kijamii yaonekane yametokea
kipindi hiki au muda mfupi uliopita ili kuleta sintofahamu.
Pamoja na tahadhari hiyo Jeshi la Polisi limesema
linaendelea kuwahakikishia wananchi kuwa kuna usalama wa kutosha tunapoelekea
kesho tarehe 29.10.2025 siku ya kupiga kura, kwani hakuna tishio lolote la
kiusalama kama walivyowahakikishia wananchi kwa taarifa waliyoitoa Oktoba 26,
2025.
Akifafanua zaidi Msemaji wa Jeshi la Polisi, David
Misime amewataka wananchi watambue kuwa habari hizo zitakazokuwa za uongo,
uzushi ni za kutaka kuchonganisha na kugombanisha ili watimize nia yao ovu
dhidi ya amani ya taifa.
"Wapo pia walioandaliwa kama ambavyo baadhi
wamesha jitokeza kuzungumza na kutoa taarifa zenye tungo tata, zenye kutaka
kuleta taharuki. Pia wanakusanya matukio ambayo yaliyotokea nchi zingine na
kuyatengeneza kwa kuyawekea sauti zenye tafauti ya kiswahili ili yaonekane
yanatokea nchini mwetu wa kati huu muhimu tunaopelekea kupiga kura kesho,"
alisema Misime.
Aidha, amesema jeshi hilo pia limebaini uwapo wa
mipango ya kuchukua picha za baadhi ya viongozi na kuziwekea maneno na sauti
zenye matamko ya upotoshaji ili ionekane wao ndio wanazungumza au wanayatamka
wakati si kweli.
Misime
amesema wakati Jeshi la Polisi
linaendelea kuwafuatilia ili wawatie nguvuni watu hao kwa mujibu wa sheria, linatoa rai
kwa wananchi watakapo ona au kutumiwa picha mjongeo na taarifa kama hizo au
vipeperushi na mengine yanayofanana na hayo wayapuuzie kwani yameandaliwa kwa
nia ovu au kinyume na lengo la kutaka kuleta taharuki kwa wananchi.
Aidha, Misime amesema wakitumiwa taarifa kama hizo
wasisambaze kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria ya ya
makosa ya kimtandao badala yake wazifute.



0 Maoni