Siku sita tu zimebaki kabla ya Watanzania kujitokeza
katika uchaguzi mkuu wa kihistoria utakaofanyika Oktoba 29. Huku kazi ya
maendeleo ikiendelea katika sekta za afya, elimu na nishati, viongozi na wadau
wa amani wanawakumbusha wananchi umuhimu wa kura kama nyenzo ya msingi ya
kulinda misingi ya Taifa.
Katika kipindi hiki cha lala salama, kauli mbiu
inayotawala ni: "Amani ni Taa, Kura ni Mafuta Yake." Kauli hii
inamaanisha kuwa bila Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura, mwanga wa
maendeleo unaweza kufifia.
Kila Mtanzania anasisitizwa kutumia haki yake ya
msingi ya kupiga kura. Kura si tu alama bali ni sauti ya maamuzi, uhuru wa
kuchagua viongozi, na maamuzi yetu ya pamoja kuhusu mustakabali wa Taifa.
"Ni haki ya kila Mtanzania kupiga kura. Kura yako
ni ya thamani sana, inajenga Tanzania yenye shule bora, hospitali za kisasa,
barabara imara na ajira kwa vijana," anasema Bi Hailat Mohamed m kazi wa
Mkuranga.
Aidha wananchi wengine wamelezea kwa kina kuhusu
sababu ya mafanikio yote ambayo Serikali inayaendeleza, ikiwemo uletaji wa
huduma bora za afya, elimu, na umeme vijijini kwamba yanatokana na uwepo wa
amani.
"Kazi inaendelea; Amani ndio nguvu yetu,"
alisisitiza Fatma Amri mkazi wa Mtwara.
Amani inatajwa kama alama ya Mtanzania kokote
ulimwenguni na mshikamano wa Watanzania. Wananchi wengi waliohojiwa wanahimiza
kulinda misingi hii, kwani "Bila amani hakuna maendeleo."
Mkazi wa Mkuranga Bw. Maulid Gomoli yeye alisisitiza
wananchi wanashauriwa kwenda vituoni Oktoba 29 kupiga kura kwa utulivu, heshima
na upendo, na kuifanya Tanzania kuwa mfano wa hekima barani Afrika.
"Kura yako ndiyo sauti ya kweli ya mabadiliko.
Tukizima taa, giza litatutawala. Oktoba 29 ni wakati wa kuongeza mwanga wa
maendeleo, kwa kura, kwa amani, kwa umoja." alisema Gomoli na kuongeza
ombi lake la kila Mtanzania kujitokeza, kupiga kura kwa maendeleo yetu, na
kulinda amani yetu. Tanzania ya Amani ni Tanzania ya Maendeleo.

0 Maoni