Raila Odinga Afariki Dunia Akiwa na Miaka 80

 

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya na Kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Bw. Raila Amolo Odinga, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.

Kifo chake kilithibitishwa leo na Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto pamoja na familia ya marehemu, wakieleza kuwa Bw. Odinga alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali moja nchini India.

Taarifa za msiba huu zimekuja huku kukiwa na uvumi uliozuka mapema wiki hii, uliodai kuwa mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa katika hali mahututi.

Hata hivyo, familia yake ilikuwa imejitokeza mapema na kuwahakikishia Wakenya kuwa hali yake ilikuwa thabiti na alikuwa akiendelea vyema na matibabu.

Seneta wa Kaunti ya Siaya na kaka mkubwa wa marehemu, Dkt. Oburu Odinga, aliwatoa hofu Wakenya kwa kusema kuwa Bw. Odinga alikuwa katika hali nzuri na alikuwa akipata nafuu nchini India baada ya kuugua ghafla.

Marehemu Raila Odinga atakumbukwa kama mmoja wa wanasiasa mashuhuri na wenye ushawishi mkubwa katika historia ya Kenya, ambaye alihudumu katika nyadhifa mbalimbali za kisiasa na kushiriki pakubwa katika harakati za mageuzi ya kisiasa nchini humo.

Chapisha Maoni

0 Maoni