Wahenga
walisema “Pori ni kitabu cha maisha, kila kipande kinasimulia hekima.” Kisha
wakaongeza kusema " Palipo na uhai, pana matumaini".
Methali
hizi za kale za Kiswahili zinapata maana yake kamili katika simulizi za
Makuyuni Wildlife Park, Hifadhi iliyo ndani ya Halmashauri ya Monduli, Mkoa wa
Arusha , ambayo kila uchwao inazidi kung’ara kama nyota ya alfajiri, ikiangaza
njia mpya za utalii na watalii pamoja na uhifadhi endelevu nchini Tanzania.
Tarehe 11
Oktoba 2025 iligeuka kuwa ukurasa wa
dhahabu katika historia ya Makuyuni. Pale ambapo Miss World China 2021, Bi
Jiang Sigi, aliwasili kwa madaha, akiwa ameambatana na walimbwende walioshinda tuzo ya Marvel Travel World
kutoka Hong Kong, Tanzania, na Kenya. Wageni hawa mashuhuri wakipokelewa kwa
bashasha na tabasamu la ukarimu na
maelezo ya kuvutia kuhusu utajiri wa wanyamapori wanaoifanya Makuyuni Wildlife
Park kuwa hifadhi ya kipekee nchini Tanzania.
Walitembea
kwenye nyasi za dhahabu za porini, wakishuhudia pundamilia wakicheza kwa
furaha, swala wakikimbia kwa ustadi, nzohe wakirukaruka mithili ya sokwe mtu
walioshiba makuzi ya mwanasayansi aliyeacha nyayo zisizofutika, Dkt. Jane
Goodall, na twiga wakinyoosha shingo zao kuelekea mawinguni kama tausi
atanuavyo mkia wake Kwa maringo. Bi Jiang Sigi alitamka kwa mshangao,
这个地方是, 颗隐藏的宝石,是全世界都应该看到的珍宝。(Kwa lugha kichina).
Maneno
yake yakitoa tafsiri ya lugha iliyokuja nchini Kwa merikebu kusema “This place
is a hidden gem, a treasure the world must see.”
Siku
iliyofuata, tarehe 12 Oktoba 2025, hifadhi hiyo ilipokea Kikundi cha Utalii
Fitness kutokea Njiro Msola Jijini Arusha kikiongozwa na Mkufunzi wa Kuafit Gym
Bw. Benson Godfrey Njiro, Arusha, kundi lenye hadhi yake katika jamii. Wakiwa
wamebeba ukakamavu wa kazi yao, waliingia Makuyuni kwa lengo la mapumziko,
lakini waliondoka wakiwa wameguswa na falsafa ya uhifadhi. Mmoja wao alisikika
akisema "Tulikuja kama walinzi, lakini tumepigwa na butwaa kama
watalii"
Kwa sasa,
Makuyuni Wildlife Park imekuwa mfano hai wa hifadhi inayopokea wageni wa kila
tabaka kutoka wageni wa kimataifa hadi wazawa wanaotafuta pumziko, elimu, na
msisimko wa asili. Kila ujio mpya ni ushuhuda wa namna Makuyuni inavyozidi
kunyanyuka, ikiimarika kama alama ya utalii endelevu na urithi wa taifa.
Makuyuni
imekuwa sio tu kivutio cha watalii, bali ni kioo kinachoakisi sura halisi ya
Tanzania yenye neema na utajiri wa vivutio vya utalii.
Na jua
linapozama nyuma ya milima ya Monduli, anga la Makuyuni hubadilika kuwa
kitambaa cha machungwa na zambarau, ishara kwamba hata giza likishuka, nyota ya
Makuyuni itaendelea kung’aa kaskazini, ikitoa mwanga wa matumaini kwa
uhifadhi wa taifa.
Na Beatus
Maganja - Arusha




0 Maoni