Wageni
kutoka mataifa mbalimbali wameendelea kumiminika kwenye banda la Hifadhi ya
Ngorongoro katika maonesho ya kimataifa ya utalii ya Magical Kenya Travel Expo
yanayoendelea jijini Nairobi, nchini Kenya, huku wengi wakivutiwa na vivutio
vya pekee vinavyopatikana katika hifadhi hiyo maarufu duniani.
Katika
maonesho hayo, wageni wameonyeshwa fursa mbalimbali za utalii na uwekezaji
zinazopatikana ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, huku kreta ya Ngorongoro
ikivutia hisia za wengi kutokana na mandhari yake ya kipekee na uwepo wa
wanyama wakubwa watano (Big Five), sambamba na historia ya kipekee ya chimbuko
la binadamu wa kale.
Afisa
Masoko Mkuu wa Hifadhi ya Ngorongoro, Bw. Michael Makombe, amesema ushiriki wao
katika maonesho hayo umefungua milango mipya ya ushirikiano wa kimataifa na
kuimarisha juhudi za kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika.
“Ushiriki
wetu katika Magical Kenya umeongeza mwamko mkubwa wa kimataifa. Wageni wengi
wameonesha nia ya kutembelea Ngorongoro na tayari tumeanza kupokea maombi ya
ziara kutoka kwa mawakala wa utalii wa kimataifa,” amesema Makombe.
Makombe
ameongeza kuwa mbali na vivutio vya asili, historia ya binadamu wa kale
inayopatikana katika Bonde la Olduvai Gorge imeendelea kuwa kivutio cha kipekee
kinachotofautisha Ngorongoro na hifadhi nyingine duniani.
Maonesho
ya Magical Kenya ni jukwaa muhimu la kutangaza vivutio vya utalii barani Afrika
na duniani kote, yakihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii wakiwemo
waendeshaji wa safari, wawekezaji, na wakala wa utalii wa kimataifa.
Na. Hamis
Dambaya – Nairobi
0 Maoni