Serikali imetoa msimamo wake wa wazi na kukemea vikali
vitendo vyovyote vya utekaji nyara, huku ikitaka wananchi kuacha kupotosha
kauli za viongozi na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Gerson
Msigwa, amesisitiza kuwa Serikali inalaani vitendo vya utekaji na vitendo
vyovyote vinavyoumiza watu.
Ndg. Msigwa ametoa wito kwa wale wanaojaribu kupotosha kauli
yake aliyoitoa alipojibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu madai ya
utekaji, waache kufanya hivyo mara moja.
“Nilichosema ni kuwa Serikali inalaani vitendo vya utekaji
na vitendo vyovyote vinavyoumiza watu. Na nimewaomba wananchi kutoa taarifa
Polisi na kutoa ushirikiano pale wanapokuwa na taarifa hizo,” amesema Ndg.
Msigwa.
Maelekezo kwa Vyombo vya Dola na Ukweli wa Kujiteka
Akifafanua kuhusu hatua za kisheria, Msemaji Mkuu ameeleza
kuwa kwa matukio yaliyotokea na kuripotiwa, Polisi wanaendelea na uchunguzi.
Amesema mamlaka husika zimeagizwa kushughulikia jambo hilo kwa ukamilifu, huku
akisisitiza:
“Wakiwabaini wahusika watakamatwa na kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria.”
Aidha, Ndg. Msigwa amesema Serikali inatambua kuwa kumekuwa
na matukio yaliyojitokeza huko nyuma ambapo baadhi ya watu walijiteka wenyewe
kwa sababu zao binafsi na kusababisha shida na taharuki kwa familia zao na
umma.
Alifichua kwamba, kulingana na takwimu za uchunguzi
zilizopita, kuna matukio yaliyotajwa kuwa ni utekaji, lakini Polisi
walipofuatilia kwa kina, walibaini haukuwa utekaji wa kweli. Ndg. Msigwa alitoa
mifano ya matukio hayo, ingawa hakuiweka hadharani.
“Nikaomba wanaofanya michezo hiyo [ya kujiteka] waache. Sasa
hapo upotoshaji upo wapi?” alihoji Ndg. Msigwa, akitaka mjadala huo uwe wa
kweli na uwazi.
Kauli hiyo inalenga kuondoa upotoshaji unaoifanywa
mitandaoni, huku ikithibitisha kwamba Serikali inachukua hatua dhidi ya
utekaji, lakini pia inatambua uwepo wa changamoto ya watu kujiteka kwa maslahi
yao binafsi, kitendo kinachoongeza mzigo kwa vyombo vya usalama na kusababisha
hofu isiyo ya lazima katika jamii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa ushirikiano wa
kutosha kwa Polisi ili kurahisisha kazi ya uchunguzi na kuwafikisha wahalifu
mbele ya sheria.

0 Maoni