Mgombea Mwenza wa Urais CCM Aendelea na Kampeni za Lala Salama Kyela

 

Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameendelea na mikutano yake ya kampeni za lala salama kwa kishindo leo Oktoba 22, 2025, katika uwanja wa mpira wa John Mwakangale, Kyela mjini, mkoani Mbeya.

Mkutano huo wa hadhara umehudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Kyela, waliokusanyika kumsikiliza Dkt. Nchimbi ambaye alitumia jukwaa hilo kueleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita na kuomba ridhaa ya wananchi kwa mara nyingine kuichagua CCM.

Dkt. Nchimbi alisisitiza kuwa serikali inayoongozwa na mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, miundombinu na uchumi wa viwanda.

Alieleza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao utaendeleza mafanikio haya na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ya mfano barani Afrika kwa maendeleo na amani.

Katika hotuba yake, alitoa wito kwa wananchi wa Kyela na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wagombea ubunge na udiwani wa CCM. Alieleza kuwa kura ya kila mmoja ni muhimu na ni silaha ya kuleta maendeleo endelevu kwa taifa.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na viongozi wa chama, wagombea ubunge na udiwani wa CCM katika jimbo hilo, ambapo walitumia nafasi hiyo kuwasilisha ahadi na mipango yao kwa wananchi. Kampeni hizi ni sehemu ya harakati za lala salama ambazo zinatarajiwa kukamilika kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu unaosubiriwa kwa hamu kote nchini.



Chapisha Maoni

0 Maoni