Baraza la
Habari Tanzania (MCT) na Uwezo Tanzania wametia saini makubaliano ya
ushirikiano wa miaka mitatu yenye lengo la kuimarisha uandishi wa habari za
elimu nchini, kuhamasisha ushiriki wa jamii katika masuala ya elimu, na kukuza
matumizi ya tafiti na ushahidi katika kuripoti stadi za maisha na maendeleo ya
kujifunza kwa watoto.
Makubaliano
haya muhimu, yaliyosainiwa leo tarehe 01 Oktoba, 2025, kati ya Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest S. Sungura, na
Mkurugenzi Mtendaji wa Uwezo Tanzania, Baraka Mgohamwende, ambao utekelezaji
wake unaanza mara moja yamelenga kuwajengea waandishi wa habari uwezo wa
kuandika habari zenye kina kimaudhui, usahihi, na mvuto ili kuchochea mijadala
ya kitaifa na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Akizungumza
kabla ya utiaji saini Sungura alisema kwamba kupitia ushirikiano huo, waandishi
wa habari wanatarajiwa kunufaika na fursa mbalimbali, ikiwemo,mafunzo ya
kitaaluma na programu za kukuza uwezo wa uhariri.
Fursa
zingine ni upatikanaji wa takwimu sahihi na ripoti za utafiti za elimu,kupata
ruzuku kwa waandishi wa habari za elimu na kuendeleza kuendeleza Tuzo ya
uandishi wa habari za elimu kupitia Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari
Tanzania (EJAT) zinazoratibiwa na MCT.
MCT
ilieleza pia Makubaliano hayo yanatilia
mkazo uandishi jumuishi kwa kuhakikisha sauti za wasichana, makundi
yaliyotengwa, na wanafunzi walioko katika mazingira hatarishi zinatambuliwa na
kupewa nafasi katika vyombo vya habari.
Baraza la
Habari Tanzania, kupitia kitengo chake cha ushauri wa kitaaluma (MICS),
kitaratibu utekelezaji wa makubaliano haya, huku kikishirikisha vyombo vya
habari na waandishi huru. Pia, Baraza litatoa majukwaa ya kusambaza tafiti za
Uwezo Tanzania na washirika wake kwa umma.
Kwa
upande wa Uwezo Tanzania, Mkurugenzi wake, Baraka amesema shirika hilo
lililojikita katika tathmini za kijamii za kujifunza na kuhamasisha sera za
elimu, kutokana na makubaliano hayo watahakikisha wanawawezesha waandishi wa
habari kuandika habari za elimu kwa weledi, kwa kutumia ushahidi, na kwa
kuzingatia usawa wa kijinsia.
Alisema
dhamira ya ushirikiano huo ni kuhakikisha kuna taarifa za kutosha za ushawishi
ili kila mtoto apate fursa ya kujifunza kwa ufanisi na kujengewa uwezo wa
kukabiliana na changamoto za maisha kupitia program za stadi mbalimbali za
maisha zinazowezeshwa na Uwezo Tanzania.
Washirika
wengine katika utekelezaji wa mradi huu wa stadi za maisha na maadili ni pamoja
na Organization for Community Development (OCODE), Milele Zanzibar Foundation
(MZF), na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University
of Dar es Salaam).



0 Maoni