Mwanaharakati na muigizaji maarufu wa filamu nchini,
Lulu Mapunda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ametoa wito kwa
wanaharakati wenzake walioko nje ya nchi kusitisha mipango na juhudi za
kuhamasisha maandamano katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga,
Lulu Mapunda alisisitiza kuwa jambo la msingi kwa sasa ni kuwapa nafasi
Watanzania kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi bila vuguvugu lolote
la maandamano ambalo linaweza kusababisha taharuki na kuvuruga amani.
"Nawaomba wanaharakati wenzangu walioko nje ya
nchi tusubiri uchaguzi upite kwanza. Tukishaona matokeo na hali ya kisiasa
imetulia, ndipo tufanye maandamano ya amani kudai katiba mpya na masuala
mengine ya msingi," alisisitiza Mapunda.
Lulu Mapunda alisisitiza kuwa uhai ni wa muhimu na
kwamba athari za maandamano ya vurugu zitawaumiza wale waliobaki nchini.
"Tukivunjwa miguu, ni ndugu zetu
watakaoshughulika na sisi, na tukiharibu nini tutafaidika nacho? Tutakao lia na
kusaga meno ni sisi tuliopo hapa," alieleza, akiongeza kuwa wanaharakati wengi wa ndani wamekimbia, kiasi
kwamba waliobaki nchini na wanaoposti Instagram ni wachache sana.
Aliongeza kuwa ni muhimu kukumbuka kuwa kila chama
kinataka dola, na hata wale walio nje wangekuwa katika nafasi ya Serikali
wangeona mapungufu kama hayo.
Muigizaji huyo aliwataka wanaharakati wote
waliokimbilia nje ya nchi, mambo yakitulia baada ya uchaguzi, warudi nyumbani
kwa ajili ya kupigania mabadiliko wakiwa nchini.
"Tukitaka kuandamana kwa amani, tuombe kibali;
hata Polisi watatulinda, lakini tupishe uchaguzi upite kwanza kwani uchaguzi
huo ulitangazwa awali," alisema na kuon geza kuwa polisi hawatakuwa tayari
kuona vurugu zinakwamisha uchaguzi, na sisi hatutafaidika kwa vurugu.
Alimalizia kwa kukumbusha kuwa mabadiliko ya kweli
hupatikana kwa njia ya kidemokrasia, na kwamba kuna ahadi za mabadiliko
zimetolewa na kama wao wataona kusubiri utekelezaji utachukua muda basi ni
vyema kuacha uchaguzi ufanyike na wan aharakati warejee nchini kufanya
maandamano kwa utulivu.

0 Maoni