Huku Taifa likipiga hatua muhimu ya kidemokrasia kwa
kufanya Uchaguzi Mkuu, utafiti wa hivi karibuni wa Kituo cha Sera za Kimataifa
Afrika (CIP–Africa) unaonyesha wazi jinsi Watanzania wanavyoendelea kuamini
katika mifumo ya kidemokrasia na mwelekeo wa maendeleo wa nchi. Matokeo ya
utafiti huu, uliochapishwa hivi karibuni, yanaakisi imani ya umma kwa
uwajibikaji na kazi inayoonekana katika sekta mbalimbali.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanyika katika mikoa
19, asilimia kubwa ya Watanzania waliohojiwa ambayo ni asilimia 83 wamesema
watashiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa leo. Idadi hii ni ishara wazi ya
ukomavu mkubwa wa kisiasa nchini na uthibitisho kuwa wananchi wanathamini na
kuamini katika mchakato wa kura kama njia halali na bora ya kufanya mabadiliko
na kuchagua viongozi wanaowataka.
Zaidi ya hayo, utafiti unaripoti kuwa asilimia 91 ya
waliohojiwa wameonyesha kuridhishwa na utendaji wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi (INEC). Hii inatoa msingi imara kwa maandalizi ya uchaguzi wa kesho,
ikionyesha kwamba wananchi wanauona mfumo unaosimamia kura kuwa wa kuaminika.
Utafiti wa CIP–Africa hauakisi tu takwimu, bali
unaakisi matokeo ya maendeleo yanayowagusa wananchi moja kwa moja. Katika
kipindi cha miaka michache iliyopita, Serikali imeelekeza rasilimali kubwa
katika sekta muhimu za afya, maji na elimu na miundombinu.
Kwenye sekta ya afya, zaidi ya hospitali 250, vituo
vya afya 1,200, na zahanati 3,000 zimejengwa kote nchini, hatua iliyoboresha
huduma za afya mijini na vijijini.Sekta ya maji imepokea uwekezaji mkubwa, huku
uimarishaji wa elimu ukiendelea kupitia mpango wa elimu bila malipo na ujenzi
wa shule mpya 1,500. Kwenye miundombinu kumekuwa na upanuzi wa barabara kuu,
madaraja, na reli ya kisasa (SGR) kazi iliyowezesha kuanza kwa fursa za ajira
na uwekezaji, na kuunganisha mikoa yote ya nchi.
Maendeleo haya yametajwa kama sababu kuu inayojenga
imani kubwa kwa wananchi. Kura ya maoni hii haikuja kama muujiza; imebeba hisia
za watu walioguswa na maboresho ya huduma za kijamii, ikionyesha ukweli wa kazi
inayoonekana na uwajibikaji.
Kutokana na utafiti huo ambao unatumika kama dira ya
Uchaguzi Mkuu wa kesho Watanzania wameeleza wazi wanachokitaka maendeleo,
utulivu na uongozi unaojali.

0 Maoni