Dkt. Samia: Vijana lindeni nchi yenu

 

Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaambia vijana nchini kwamba Tanzania yao ni mahali pazuri na kuwasihi wasidanganyike kuiharibu nchi yao.

Dkt. Samia amewaambia vijana kwamba Tanzania ni pepo ukilinganisha na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika na Afrika ya Kati.

Mgombea huyo wa urais kupitia CCM ameyasema hayo jana Oktoba 23, 2025 alipohutubia mkutano mkubwa wa kuhitimisha kampeni zake Mkoani Dar es Salaam uliofanyika katika Viwanja vya Tanesco Vituka wilayani Temeke.

Mkutano huo ulioshirikisha majimbo ya Temeke, Mbagala, Chamazi na Kigamboni, ulikuwa wa mwisho kwa kampeni zake Tanzania Bara, akiwa amefanya ziara za kampeni katika mikoa yote 26 ya Bara. Amabpo leo Oktoba 24, 2025 Dk Samia atahitimisha kampeni zake Tanzania.

Zanzibar kwa kuhutubia wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwenye Viwanja vya Kibandamaiti.

"Kwenye nchi yenye jina, yenye sifa zake yenye kuendeleza watu wake, msidanganywe wale waliopo nje huko wasiwadanganye, hapa ni pazuri kwelikweli mkipata fursa tu ya kuingia kwa majirani zetu

hapo, kaangalie vijana wenzenu wanavyokula ndumu unaweza ukasema mimi narudi Tanzania," Dkt. Samia aliwaambia maelfu ya wananchi wakiwamo vijana wa majimbo hayo.

Ameongeza: "Tanzania ndio kwetu, kwa hiyo niwaambie vijana sisi wazazi wenu tunapita, nchi hii inawategemea ninyi, tunatarajia ninyi (vijana) tuwaachie nchi hii muiendeshe kama tunavyoiendesha.

Kwahiyo vijana wa Tanzania msidanganywe hata kidogo na katika kuendesha nchi tumetengeneza mifumo mizuri sana ambayo kila baada ya miaka mitano tunachaguana namna ya kuongoza nani ashike nafasi gani, katika ngazi tofauti, hakuna maeneo mengine wanangu".

Amewataka vijana kutuliza munkari kwani nchi ni mali yao na hakuna mwenye cheti cha kusema ni yake.

"Wengine wanasema sisi tunawakilisha wananchi, wananchi ni kina nani, wananchi ni ninyi hapa na wengine na wengine na wengine, hakuna mwenye milki ya wananchi. Hapa tunapeana majukumu tu we shika jukumu hili, wewe hili, kwa hiyo nawaomba vijana wangu msiharibu nchi yenu, msiharibu amani ya nchi yenu fuateni serikali yenu inavyowaelekeza, fuateni, Katiba yenu inavyowaelekeza, fuateni sheria za nchi zinavyowaambia, zinavyotaka, mtaishi kwa salama, mtaishi kwa amani hamtasumbuliwa," amesema Dkt. Samia.

Amesisitiza wote waliojiandikisha kupiga kura, wakapige kura Oktoba 29, mwaka huu bila hofu.

 "Mama yuko macho anawalinda, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo macho vinawalinda. Kama yamewashinda wao sisi tupo tunaendelea na ujenzi wa nchi yetu," amesema Dkt. Samia aliyetumia dakika 30 kuhutubia mkutano huo.

Aidha, amesema mkutano huo umehudhuriwa na vyama rafiki ambavyo amesema vimekuja nchini kusoma ili wakati wa uchaguzi na wao wakafanye vipi Kwa vile CCM ni chama kikubwa na ndio maana wapo hapa.

Alivitaja vyama rafiki vilivyowaunga mkono ni SWAPO cha Namibia, Chama Cha Kikoministi cha China, ANC cha Afrika Kusini, na NRM cha Uganda.

Akigusia falsafa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisema ili tupate maendeleo tunahitaji mambo manne - watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

 Alifafanua kuwa CCM katika miaka mitano ijayo itajikita zaidi katika masuala hayo ikiwemo watu kwa ajili ya kusimamia utu wa mtu, utu wa Mtanzania katika kupata chakula, huduma za afya, maji safi na salama,

umeme na makazi ambavyo yote yamefanyiwa kazi.Alisema kisichoguswa ni makazi lakini watu binafsi wanajenga, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linajenga nyumba nchi nzima ili kuwapatia makazi bora watu.

Alisema katika uchumi wamefanya vizuri katika uchumi mkubwa na uchumi mdogo.

Naye Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha- Rose Migiro amesema Dkt. Samia amekuwa bingwa wa sekta ya sanaa, ubunifu na michezo nchini, ambako amekuwa akinunua bao kwa michuano ya kimataifa maarufu Goli la Mama.

Naye Mwenyekiti wa UWT Taifa na Mratibu wa kampeni Kanda ya Dar es Salaam, Mary Chatanda alisema ametumwa na wanawake wa Tanzania karibu milioni 15.7, kuwa wapo tayari kumpa kura za kishindo Dkt. Samia kutokana na kuliheshimisha taifa kwa miaka minne aliyokaa madarakani kwa kuleta maendeleo makubwa katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahamoud Thabiti Kombo amesema Dkt. Samia anafanya kazi Kwa vitendo sio maneno, katika kuleta maendeleo na ajira kwa vijana ndani na nje ya nchi.

Amesema leo wamepata mkataba wa ajira 50,000 za Watanzania hususani vijana kwenda kufanya kazi nje ya nchi huku nyingine 20,000 zipo njiani zinakuja.

Na, Aboubakary Liongo -Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM

Chapisha Maoni

0 Maoni