Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekanusha taarifa
zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa taasisi hiyo imechapisha
fedha na kuzisambaza kwa ajili ya kugharamia uchaguzi mkuu, ikibainisha kuwa
madai hayo hayana ukweli wowote bali ni upotoshaji unaolenga kupotosha umma.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Ijumaa,
Oktoba 17, 2025 na kusainiwa na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, benki hiyo
imesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakihamasishwa kuondoa fedha zao
kwenye benki za biashara kwa madai kuwa zinaishiwa fedha kutokana na uchaguzi.
Hata hivyo, BoT imesisitiza kuwa taarifa hizo ni
za uongo na zinapaswa kupuuzwa.
“Ninapenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa
taarifa hizo si za kweli, zinapaswa kupuuzwa na kukemewa wote wanaozisambaza,”
imesema BoT.
BoT imefafanua kuwa, kama ilivyo katika nchi
nyingine duniani, uchapishaji wa fedha hufanywa kwa mujibu wa sheria. Kwa
mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, Sura ya 197, taasisi hiyo ina
jukumu la kuzungusha kiasi cha fedha kinachohitajika katika shughuli za
kiuchumi pamoja na mahitaji ya kubadilisha fedha zilizochakaa.
Aidha, benki hiyo imeeleza kuwa fedha huingizwa kwenye mzunguko kupitia benki za biashara na si vinginevyo, na kwamba mchakato huo hufanyika kwa kufuata taratibu rasmi ili kuhakikisha sera za fedha na utulivu wa bei unadhibitiwa ipasavyo.

0 Maoni