WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka balozi wa Tanzania
Nchini Japan Anderson Mutatembwa kusimamia utekelezaji wa sera ya mambo ya nje
ikiwa ni pamoja na kudumisha diplomasia ya uchumi kwa kuhamasisha uwekezaji na
upatikanaji wa masoko wa bidhaa za ndani.
“Ni jukumu lako kwenda kutangaza fursa zilizopo hapa nchini,
tumia vizuri mahusiano yetu na Japan kupata wawekezaji katika maeneo
mbalimbali, zipo fursa nyingi ambazo tunahitaji kuzipata hasa za kiuchumi,
ukifika huko weka mpango wa kutembelea wawekezaji, yapo maeneo ambayo
tunahitaji kunufaika.”
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumatatu, Septemba 08, 2025)
alipokutana na Balozi huyo ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa pia amemtaka Balozi Mtatembwa kuweka mpango
wa kuwaunganisha Watanzania waishio nchini japan na kuwahamasisha kushiriki
katika fursa mbalimbali ya kiuchumi zilizopo nchini humo jambo ambalo
litaiwezesha Tanzania kunufaika na hatua hizo.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Balozi Mutatembwa kutangaza
vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza idadi ya watalii
wanaoitembelea Tanzania. “Tumia majukwaa mbalimbali kuhamaisha Wajapan kuja
kuitembelea Tanzania, lengo letu ni kuhakikisha tunaongeza idadi ya watalii
nchini.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka balozi
huyo kuweka mikakati zaidi ya kuitangaza lugha ya kiswahili nchini humo. “Ukiwa
huko jitahidi kupanua wigo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili.”
0 Maoni