Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imezitaka taasisi na
asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa
uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi na weledi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhani leo tarehe 08 Septemba, 2025 wakati
akiufungua kikao kazi cha Tume na taasisi na asasi hizo kilichofanyika Mkoani
Dodoma.
”Ni vyema mkafahamu kuwa kifungu cha 10(1)(g) na (h) cha
Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 na kanuni ya 22 na
23 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024, zimeipa Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi mamlaka ya kutoa elimu ya mpiga kura nchini, kuratibu na
kusimamia taasisi na asasi zinazotoa elimu hiyo. Hivyo, kazi mnayoenda kuifanya
ni moja ya majukumu ya kisheria ya Tume na mnapaswa kuifanya kwa weledi na
ufanisi mkubwa,” amesema.
Ndugu Kailima ameongeza kuwa, Tume inatarajia kuona kuwa,
taasisi na asasi za kiraia zinatoa elimu iliyolengwa haswa kwa kutoa kipaumbele
kwenye mambo ambayo yatawapa wananchi, wagombea na vyama vya siasa kwa ujumla
uelewa wa namna ya kushiriki kwenye kampeni kwa amani na utulivu ikiwa ni
pamoja na kupata uelewa mzuri wa utaratibu wa kupiga kura.
”Hatutarajii kabisa mtoe elimu ambayo italeta mkanganyiko
kwenye jamii na kuiingiza nchi kwenye machafuko kama ilivyotokea katika maeneo
mengine hapa Afrika na duniani kwa ujumla,” amesema.
Amesisitiza kuwa taasisi na asasi hizo haziruhusiwi kuwapa
watu wengine au taaisi au asasi nyingine vibali
walivyopewa na kwamba vibali hivyo ni lazima vitumiwe na walengwa tu.
”Nyie ndio mabalozi wa Tume, hivyo, mhakikishe katika
kipindi chote cha utekelezaji wa jukumu lenu la kutoa elimu, mnazingatia
Katiba, sheria, kanuni na maelekezo ambayo Tume imekuwa ikiyatoa mara kwa
mara,” amesema.
Kikao kazi hicho kiliwaleta pamoja viongozi wa Tume na
wawakilishi wa taasisi na asasi 164 zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga
kura ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa.
Mada zilizowasilishwa ni pamoja na Mwongozo wa Elimu ya
Mpiga Kura wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025, Sheria za
Uchaguzi, Kura ya Rais Portal (Kura ya Rais Popote) na Mchakato wa Uchaguzi.
0 Maoni