Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (MB) kufanya ziara rasmi nchini
Uingereza kuanzia tarehe 08 hadi 12 Septemba 2025, inayolenga kuendeleza na
kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na wa muda mrefu baina ya Tanzania na
Uingereza.
Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri Kombo pamoja na
mambo mengine, atakuwa Mgeni Rasmi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa kituo kipya cha
Taasisi ya ODI Global inayojihusisha kufanya tafiti kuhusu maendeleo
utakaofanyika Westminster, London Septemba 09, 2025.
Katika ziara hiyo ambayo inaelezwa inafanyika baada ya
takribani miaka 14 tangu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania alipofanya ziara
mara ya mwisho nchini Uingereza. Katika ziara hiyo Mhe. Waziri Kombo pia
atakutana na kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi waandamizi wa
Serikali ya Uingereza, Jumuiya za kimataifa, Taasisi za Kifedha, wawakilishi wa
kampuni za uwekezaji na wafanyabiashara kwa lengo la kuhamasisha na kutangaza
uwekezaji, biashara na utalii nchini Tanzania.
Viongozi wa Serikali na taasisi za kimataifa ambao Waziri
Kombo atakutana nao ni pamoja na Mheshimiwa Lord Collins wa Highbury, Waziri wa
Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika; Mheshimiwa Kerry McCarthy (MB),
Waziri wa Uingereza anayeshughulia Masuala ya Tabianchi; Mheshimiwa Shirley
Ayorkor Botchwey, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola; na Mheshimiwa Arsenio
Dominguez, Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Bahari (IMO).
Taasisi za kifedha na uwekezaji ambazo Waziri Kombo
atakutana na viongozi wake ni pamoja na British International Investment (BII),
UK Export Finance (UKEF), King’s Foundation na kushiriki katika meza ya
majadiliano ya kibiashara na kampuni teule za Uingereza ili kutangaza fursa za
biashara, uwekezaji, nishati safi, miundombinu, na sekta nyingine za kipaumbele
zinazopatikana nchini.
Ziara hiyo inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano
wa muda mrefu kati ya Tanzania na Uingereza kwa kufungua fursa mpya katika
biashara, uwekezaji, mabadiliko ya tabianchi, ubunifu pamoja na kuimarisha
ushirikiano wa kimataifa ndani ya Jumuiya ya Madola.
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
0 Maoni