Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA
imefanikiwa kumkamata simba jike akiwa hai baada ya mfululizo wa mashambulizi
ya wanyama hao kuua zaidi ya mifugo 20 katika Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma.
Simba huyo aliingia kwenye rada za askari wa TAWA majira ya
saa 4 usiku, Septemba 6, 2025, katika kijiji cha Chemchem, kufuatia msako mkali
uliodumu kwa siku tatu ambapo mnyama huyo alijikuta tayari amenasa katika mtego maalum uliowekwa na Askari hao.
Imeripotiwa kuwa wanyama simba wamekuwa wakifanya
mashambulizi ya mifugo katika vijiji vya Chemchem na Iyoli, Kata ya Kingale
ambapo katika nyakati tofauti waliua ng’ombe wawili na punda mmoja na baadae
kuua ng’ombe 18 katika gereza la king'ang'a. Aidha, waliripotiwa pia
kuua mbuzi wawili katika kijiji cha Iyoli.
Kutokana na ongezeko la matukio hayo, Mamlaka ilianza
operesheni ya kudhibiti simba hao kwa kutumia
Askari wake na baadaye kuongeza
timu ya madaktari wa wanyama. Hatimaye, mnamo septemba 6 majira ya saa 4 usiku,
simba jike alikamatwa kwa kutumia mbinu za kitaalamu.
Afisa Mhifadhi Daraja la Kwanza ambaye pia ni daktari wa
wanyamapori Masalu Makoye Mroje, alisema simba huyo atasafirishwa kwenda eneo
la mbali lenye mazingira rafiki, ili kuzuia madhara kwa wananchi na mifugo yao.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Chemchemi, Kata ya
Kingale, wilayani humo, wameipongeza Serikali kupitia TAWA kwa uwajibikaji wake
katika kukabiliana na changamoto za wanyamapori waharibifu, hususan kitendo cha
kumdhibiti simba huyo aliyezua taharuki kwa wananchi.
"Tumekuwa na changamoto ya wanyamapori wakali na
waharibifu Kwa muda sasa, Simba walikula mifugo yetu na kutusumbua lakini leo
amani imerejea baada ya TAWA kufanikiwa kumdhibiti mnyama huyu na kutuahidi kufuatilia
Simba wengine ili kuwaondoa kijijini kwetu" alisema Mwenyekiti wa Kijiji
cha Chemchem Bw. Mashaka Said Funga.
Aidha, TAWA inaendeleza uchunguzi na ufuatiliaji ili kubaini kama kuna simba wengine katika maeneo hayo ili waweze kuondolewa, na kuwaomba wananchi kutoa taarifa haraka iwapo watawaona.
0 Maoni