Umoja wa Mataifa wa Sayansi ya Jiolojia (IUGS) kwa
kushirikiana na Mtandao wa jiopaki duniani (GGN) umetambua maeneo ya Jiopaki
yanayofanya vizuri katika uhifadhi ambapo eneo la hifadhi ya Ngorongoro kupitia
Kreta ya Ngorongoro ni moja la eneo lililotambuliwa kwa uhifadhi wa
wanyamapori, mifumo ya ikolojia na uthibiti wa mimea vamizi hali inayofanya
eneo hilo kuwa salama.
Utambuzi wa maeneo hayo umetangazwa katika mkutano wa 11 wa
kimataifa wa Hifadhi za Jiolojia za UNESCO unaofanyika Mji wa Araucania nchini
Chile kuanzia tarehe 8-12 Septemba, 2025 ambao mkutano huo umezikutanisha
jiopaki zote duniani Ngorongoro ikiwa ni sehemu ya mkutano huo.
Tanzania kupitia Hifadhi ya Ngorongoro imeshiriki mkutano
huu kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika kusimamia na kuendeleza Hifadhi ya
Jiolojia ya Ngorongoro Lengai ambayo ni jiopaki pekee iliyopo kusini mwa Jangwa
la Sahara na ya pili barani Afrika ikitanguliwa na Jiopaki ya M’Goun ya nchini
Morocco.
Katika Mkutano huo Hifadhi ya Ngorongoro imewakilishwa na
Afisa Uhifadhi Mkuu na mtaalam wa urithi wa Utamaduni Dkt. Agnes Gidna aliyetoa
maada ya uzoefu wa kusimamia na kuendesha Jiopaki ya Ngorongoro Lengai pamoja
na Afisa Uhifadhi kutoka idara ya Maendeleo ya Jamii Lightness Kiyambile
aliyewasilisha mada kuhusu ushiriki wa Jamii na namna wanavyonufaika na uwepo
wa Jiopaki ya Ngorongoro.
Eneo la hifadhi ya Ngorongoro lilitambuliwa na UNESCO na kupewa hadhi ya kuwa Geopark mwaka 2018 ambapo katika mkutano huo NCAA imepata fursa ya kuhamasisha nchi nyingine kufuata nyayo zake katika uanzishaji wa hifadhi za jiolojia, ikiendelea kuwa mfano wa kuigwa na kinara wa uhifadhi endelevu barani Afrika.




0 Maoni