Mkimbiza
Mwenge Kitaifa 2025 Ndugu Ismail Ali
Ussi amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Geita pamoja na Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoani humo muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa
barabara ya Kasco.
Amesema
kilio cha wananchi wa Geita kuhusu changamoto za miundombinu kinaendelea kupata
majibu ya vitendo. “Leo, katika eneo la Kasco hadi Shule ya Sekondari Nyanza,
Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa
barabara ya lami nyepesi yenye urefu wa kilomita 1.32, hatua inayoongeza chachu
ya maendeleo kwa wakazi wa Manispaa ya Geita.”
Mradi huo
unaotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Geita kupitia fedha za mapato ya
ndani, unasimamiwa na TARURA Geita huku mkandarasi akiwa ni kampuni ya Evax
Construction Ltd ya Mureba. Kwa mujibu wa mkataba namba 63CC1/2924/2025/W/03,
gharama ya ujenzi ni shilingi 999,950,000.00.
Kwa mujibu
wa taarifa ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita, Mhandisi Bahati Subeya, mradi
huo ulianza Machi 7, 2025 na unatarajiwa kukamilika Septemba 8, 2025. Hadi sasa
umefikia asilimia 95 ya utekelezaji, ambapo zaidi ya shilingi milioni 754
zimeshalipwa.
Mhandisi
Subeya amesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, yakiwemo
kupunguza adha ya usafiri wakati wote wa mwaka, kuchochea biashara na kuboresha
mandhari ya mji.
Baada ya
kukagua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndg.
Ismail Ali Ussi, alisifu ubora wa utekelezaji akisema hakuna chembe ya
ubabaishaji.
“Nimetembea mikoa 24, huu ni mkoa wa 25.
Sikuwahi kuona miradi ya kiwango cha juu kama hii inayotekelezwa na TARURA.
Jana nilizindua barabara ya Nzera, leo Kasco, yote kwa ubora wa hali ya juu.
Hakuna harufu ya ufisadi, hakuna ubabaishaji – kazi hii inastahili saluti,”
amesema Ussi huku akishangiliwa na wananchi.
Aliongeza
kuwa miradi inayotekelezwa chini ya usimamizi wa TARURA ni ushahidi kuwa kodi
zinazotozwa kwa wananchi zinatendewa haki.
Pia
aliipongeza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Geita kwa kuendelea
kulinda amani, jambo lililompa faraja kubwa katika ziara hiyo ya Kitaifa.
0 Maoni