Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha
Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amewaeleza wananchi wa Bukombe kuwa
maendeleo yaliyopatikana jimboni humo yametokana na upendo wa Rais Samia Suluhu
Hassan kwao, hivyo wajitokeze kuwapigia kura wagombea wa CCM ifikapo Oktoba 29
mwaka huu ili waendelee kupata maendeleo.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 16, 2025 katika mkutano wa
kampeni uliofanyika Kata ya Runzewe Magharibi wilayani Bukombe mkoani Geita
ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali inayoongozwa
na Rais Samia Suluhu Hassan chini ya CCM imefanya kazi kubwa ya kuleta miradi
ya maendeleo katika Kata hiyo ambayo miundombinu yake imefunguka zikiwemo
ujenzi wa barabara, shule, miradi ya maji. Ameutaja mradi wa Msasa ambao upo mbioni kupanuliwa ili
kuhudumia wananchi wengi zaidi.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho wamejenga Ofisi mpya ya
Halmashauri ya Wilaya, soko na stendi ya kisasa ili kusogeza na kuboresha
huduma za jamii.
“ Wilaya yetu ina shule tano za kidato cha tano na sita, tunajenga Chuo Kikuu kimoja Bukombe, tumejenga maghala. Nataka niwaambie mkituchagua tunaongeza sekondari nyingine ili watoto wanaozaliwa hapa wapate elimu katika ngazi zote,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Kazi yenu wananchi ni kupiga kura ili mtudai
maendeleo, Rais Samia anatupenda wananchi wa Runzewe, anatupenda wananchi wa
Bukombe hivyo, tarehe 29 Oktoba tujitokeze kwa wingi na tumchague yeye katika
nafasi ya urais.”
Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Runzewe Magharibi, Patrick
Isongolo amesema Rais Samia na Dkt. Biteko wamefanya jitihada kubwa ya kuleta
maendeleo katika Kata hiyo hivyo Oktoba 29 wananchi wakawachague wagombea wa
CCM.
“ Mwaka jana Biteko amechangia ujenzi wa kituo cha afya,
tulikuwa na changamoto kubwa sana ya barabara na daraja pale kwa Sae, Dkt.
Biteko na Serikali ya CCM wamesaidia kuhamasisha na kutuletea maendeleo
tunayoyashuhudia,” amesema Isongolo.
Katika hatua nyingine,
akizungumza katika Kata ya
Runzewe Mashariki Dkt. Biteko
amesema Rais Samia angependa
kuona wananchi wanapata maendeleo ya haraka katika viwango vya juu.
Amefafanua kuwa Rais Samia alitoa fedha za kukamikisha
ujenzi wa zahanati na Kituo cha Afya cha Msonga pamoja na kujenga kituo kingine
cha afya na shule.
“ Nasimama hapa kuwatangazia barabara ya pale kona nne
tutakarabati ili watu wapite vizuri, ninemwambia diwani atafute eneo tununue
ili tujenge shule watoto wapate mahali pa kusoma,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa wamedhamiria kufikisha umeme katika kila
kitongoji cha Kata hiyo ya Runzewe Mashariki.
Aidha, amewaasa kuwa hakuna maendeleo yatakayotokea bila wao
kujitokeza na kupiga kura kumchagua mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
mbunge Biteko na Mary diwani.
“ Wapiga kura waliopo hapa ni 17,006, uchaguzi huu ningeomba
twende wote tukapige kura,” amesema Dkt. Biteko.
Naye, Diwani wa Kata ya Runzewe Mashariki, Mary Nchiba
amewaomba wananchi wa Kata hiyo kuwapigia kura wagombea wa CCM kwa kuwa
wamefanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo.
0 Maoni