Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeandaa kambi
maalumu ya kuondoa mawe kwenye njia ya mkojo kwa kutumia teknolojia ya kisasa
ya Leza ambapo takribani wagonjwa 20 watanufaika na huduma hiyo ambayo
itafanyika kuanzia Septemba 22 hadi 26, 2025.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji MNH-Mloganzila,
Dkt. Godlove Mfuko amesema kambi hiyo itafanywa na wataalam wa Hospitali ya
Taifa Muhimbili-Upanga na Mloganzila kwa kushirikiana na wataalam wa MediAfric
Tanzania.
Huduma hii ya kisasa hutumia kifaa maalum kinachopita
kupitia njia ya mkojo kufika kwenye figo ambapo kwa msaada wa mashine ya kisasa
ya leza, mawe huvunjwavunjwa na kutolewa bila kufanya upasuaji wa wazi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mfuko watakaonufaika na huduma hii ni
wale wenye changamoto za mawe kwenye figo yanayojirudia, mawe yanayoshindikana
kuondolewa kwa tiba ya kawaida au yale ambayo hayafai kutibiwa kwa njia ya
extracorporeal shockwave lithotripsy (ESWL).
Hivyo kwa wagonjwa wenye changamoto hiyo, wanashauriwa
kufika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila kwa ajili ya kuwekwa
kwenye orodha ya kuweza kupata matibabu hayo.

0 Maoni