Wizara ya Maliasili na Utalii imeahidi kuendeleza ushirikiano na taasisi zote zinazounda mnyororo wa haki jinai ili kuhakikisha ukamataji, upelelezi na uendeshaji wa mashtaka unafanyika kwa weledi na ufanisi mkubwa katika kulinda rasilimali za taifa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara anayeshughulikia Uhifadhi,
Kamishna wa Polisi (CP) Benedict Wakulyamba ametoa kauli hiyo jijini Arusha
alipokuwa akifunga mafunzo ya kikazi kwa majaji, wadau wa haki jinai na Shirika
la Hifadhi za Taifa (TANAPA) yaliyolenga kuimarisha uhifadhi endelevu wa
maliasili.
CP Wakulyamba amesema changamoto zinazokabili sekta ya
uhifadhi, ikiwamo vitendo vya ujangili, uvamizi wa mifugo ndani ya hifadhi na
migongano kati ya binadamu na wanyamapori, zinaendelea kushughulikiwa kwa
mikakati madhubuti.
“Miongoni mwa hatua tunazochukua ni kutoa elimu ya uhifadhi,
kuimarisha uwajibikaji wa watendaji, na kufanya upelelezi wa kesi za ujangili
kwa weledi mkubwa na kwa kuzingatia sheria zilizopo,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa Wizara itaendeleza mafunzo ya aina
hiyo katika kanda mbalimbali za uhifadhi, hususan maeneo yenye mahakama,
sambamba na kushirikisha taasisi zote za mnyororo wa haki jinai ili kuongeza
uelewa wa sheria za uhifadhi nchini.
Hata hivyo, CP Wakulyamba amesema Wizara haitasita kuchukua
hatua hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa watumishi wake na taasisi za
uhifadhi zitakazobainika kushirikiana na wahalifu kuhujumu maliasili.
Ameishukuru Mahakama ya Tanzania chini ya uongozi wa Jaji
Mkuu kwa kuruhusu mafunzo hayo kufanyika pamoja na washiriki wote waliotoa
mchango wao.
Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Steria Raphael
Ndaga, amesema mafunzo hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa yamewaleta
pamoja wadau muhimu wa serikali wenye jukumu la kulinda na
kusimamia maliasili.
Na. Sixmund Begashe - Arusha



0 Maoni