Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano ambaye pia ni Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja,
amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika
kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa umma, ili kusaidia utekelezaji wa haki
ya wananchi ya kupata taarifa.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha Kamati
hiyo, kilichowakutanisha wajumbe kutoka idara na vitengo mbalimbali vya wizara
hiyo, Bw. Mwaipaja alisema lengo kuu ni kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa
matumizi ya umma.
"Wizara ina jukumu la msingi la kuwapatia wananchi
taarifa kuhusu sera, mipango, programu na matukio mbalimbali ya kisekta, ili
kuwawezesha kuelewa majukumu ya wizara na mchango wake katika maendeleo ya
nchi," alisema Bw. Mwaipaja.
Aliongeza kuwa wajumbe wa kamati hiyo wanapaswa kutoa
ushirikiano wa karibu kwa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa kuwasilisha
kalenda za matukio muhimu mapema, ili kurahisisha uratibu na upashanaji taarifa
kwa njia mbalimbali.
"Napenda kusisitiza kuwa taarifa mnazozitoa si tu
kwamba zinasaidia kuandaa majarida ya wizara, bali pia hutumika kwenye tovuti
ya wizara, mitandao ya kijamii kama Instagram, WhatsApp, Twitter, LinkedIn,
Hazina TV na hata kwenye vyombo vya habari vya kitaifa kama runinga na
magazeti," alisema.
Aidha, alieleza kuwa tayari wizara imetoa toleo la nne la
Jarida la Hazina Yetu, ambalo linasheheni taarifa mbalimbali muhimu kwa
wananchi, huku maandalizi ya toleo la tano yakiwa yanaendelea, yakitegemea
taarifa kutoka katika idara na vitengo vya wizara.
Bw. Mwaipaja alisema kuwa kupitia matumizi ya lugha nyepesi
na yenye kueleweka, majarida hayo yamekuwa yakipokelewa vyema na wadau
mbalimbali wa ndani na nje ya wizara, ambao sasa wameonyesha nia ya kuendelea
kushiriki kikamilifu katika mchakato wa upatikanaji na usambazaji wa taarifa.
Katika hatua nyingine, aliwataka wajumbe hao kuendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na wizara, kwa ajili ya kuongeza maarifa, kufanya tafiti za kitaaluma na matumizi mengine yenye tija kwa jamii.
0 Maoni