Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wanachama na
viongozi wa chama hicho waliogombea nafasi mbalimbali kuvunja makundi na
kuungana na walioteuliwa, ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM katika
Uchaguzi Mkuu ujao.
Akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Septemba 5,
2025 katika Viwanja vya Sabasaba, mjini Njombe, Dkt. Samia ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliwataka wanachama waliopitishwa na waliokosa uteuzi
kuweka tofauti zao pembeni kwa maslahi ya chama.
“Nampongeza Mwenyekiti Deo Sanga kwa kauli yake thabiti ya
kuvunja makundi. Huu ndiyo mwelekeo tunaoutaka. Makundi yote yavunjwe, sasa ni
wakati wa mshikamano kwa ajili ya ushindi wa CCM kote nchini,” alisema Dkt.
Samia.
Kauli hiyo imekuja baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Njombe, Deo Sanga maarufu kama Jah People, kutoa wito kwa wagombea wote
kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha ushindi wa chama kuanzia ngazi ya urais,
ubunge hadi udiwani.
“Mwenyekiti, mimi tayari nimewaambia wagombea kwamba makundi
nimeyavunja. Nimewaonya, mtu asije akaniambia fulani hakukubali au fulani
hakupitishwa. Uchaguzi umekwisha, sasa kazi ni moja tu kutetea ushindi wa chama
chetu,” alisema Sanga.
Sanga hakuteuliwa kuwania tena ubunge wa Jimbo la Makambako,
nafasi iliyochukuliwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Daniel Chongolo, lakini
ameonyesha mfano wa kukubali maamuzi ya chama na kusisitiza mshikamano.
Vituo 50 vya
Kuhifadhi Parachichi Kujengwa
Katika hatua nyingine, Dkt. Samia alitangaza mpango wa
Serikali wa kuanzisha vituo 50 vya kuhifadhia zao la parachichi katika mikoa
inayolima zao hilo kwa wingi, likiwemo eneo la Nyanda za Juu Kusini.
Alisema kati ya vituo hivyo, viwili vitajengwa katika Wilaya
ya Rungwe, mkoani Mbeya, ili kuhakikisha zao hilo linaweza kuhifadhiwa wakati
bei ya soko la dunia ikiwa juu, hivyo kuongeza kipato kwa wakulima.
“Tutaweka pia maofisa ugani maalum watakaoshughulikia zao la
parachichi, hasa katika mikoa ya Njombe na Mbeya, kuhakikisha wakulima wanapata
elimu ya kitaalamu ya uzalishaji,” alieleza.
Serikali Kuwachukulia Hatua Wenye Mashamba ya Chai
Wasiyoendeleza
Dkt. Samia aliwaonya wawekezaji waliomiliki mashamba makubwa
ya chai ambayo hayaendelezwi, akisema Serikali haitasita kuyachukua.
Alisisitiza kuwa wawekezaji hao watalazimika kulipa madeni wanayodaiwa na
wakulima pamoja na wafanyakazi wao kabla ya mashamba hayo kuchukuliwa.
Msisitizo kwa
Maendeleo ya Viwanda na Kilimo
Katika hotuba yake, Rais Samia pia alieleza dhamira ya Serikali kuendeleza mpango wa kuanzisha kongani za viwanda katika kila wilaya nchini, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo kwa kutoa ruzuku zaidi kwa wakulima.
“Tunaendelea kuweka mazingira bora kwa ajili ya uzalishaji
wa kilimo na viwanda. Hii ni sehemu ya mkakati wetu wa kuinua uchumi wa mtu
mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” alisema.
Kampeni Zaendelea
Iringa
Baada ya mikutano hiyo ya Njombe, Dkt. Samia ameendelea na kampeni zake mkoani Iringa, ambako leo anatarajiwa kuhutubia wananchi katika maeneo ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Nyololo na Kalenga.
Na. Aboubakary Liongo - Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM
0 Maoni