Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ibada ya
mazishi ya Askofu Mstaafu Dkt. Martin Fatael Shao aliyefariki Dunia Agosti 25,
mwaka huu.
Akizungumza katika ibada ya mazishi Septemba 4, 2025
yaliyofanyika katika kijiji cha Lole, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro Dkt.
Biteko amesema Hayati Askofu Shao wakati wa uhai wake alifanya mambo mengi
mazuri ya kukumbukwa hata baada ya kifo chake.
“ Mzee wetu, Hayati Askofu Shao ameanza kazi za kanisa akiwa
kijana na amefanya kazi kubwa ambayo kila mmoja anaishuhudia leo, ameacha alama
inayotokana na kazi aliyoifanya,” amesema
“Mheshimiwa Rais amenituma niwaletee salamu zake za pole
nyingi sana Wanafamilia, Viongozi wote wa Kanisa KKKT pamoja na ndugu jamaa na
marafiki wote kwa na msiba,” amesema
Amesema Serikali itakumbuka mchango wa Askofu Shao ambaye
ametumikia Kanisa katika maisha yake tangu ujana wake na hata baada ya kustaafu
ameendelea kuwa mshauri.
Amewahimiza waombolezaji kuendelea kuwa karibu na
kushirikiana na wafiwa katika kipindi
hiki cha majonzi huku akiwahakikishia kuwa Serikali iko pamoja nao hasa katika
kipindi hiki cha majonzi.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania KKKT, Dkt. Alex Malasusa amewataka waumini kutumia msiba huu
kumshukuru Mungu kwa ajili ya mtu kama hayati Askofu Shao ambaye alikuwa
kielelezo cha maisha bora kwa wanadamu.
Ameongeza kuwa Hayati Askofu Shao akikuwa mnyenyekevu na
msikivu hali ambayo amesema imeanza kutoweka miongoni mwa wanajamii.
“wanyenyekevu kama Dkt. Shao wameanza kuwa hadimu katika jamii na Viongozi waliomtengeneza Hayati Dkt. Shao walifaulu sana… amefanya mambo mengi ndani na nje ya usharika,” amesema Askofu Dkt. Malasusa.
Amefafanua kuwa Askofu Shao enzi za uhai wake akifanya kazi
kubwa ya uinjiliahaji ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa umahiri mkubwa.
“ Tusizoee misiba, kila msiba utupe nafasi ya kutafakari
maisha yetu,” amesema Askofu Malasusa.
Ibada ya mazishi imehudhuriwa na maelfu ya waombolezaji na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Mkuu wa Mkoa wa Kilimajaro, Nurdin Babu na Mgombea wa Urais kwa tiketi ya CHAUMMA, Salum Mwalimu.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni