WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amelipongeza Jeshi la Magereza Tanzania kwa kufanya urasimishaji wa
ujuzi wanaoupata wafungwa kupitia VETA na kuwawezesha kupata ajira au kuanzisha
biashara zao baada ya kumaliza kifungo.
Ameongeza kuwa kupitia mitaala mipya ya mafunzo ya amali na
stadi za kazi, jeshi hilo limefanikiwa kuwanufaisha zaidi ya wafungwa 5,000
ambapo baadhi yao wameweza kujiajiri au kuajiriwa baada ya kumaliza vifungo vyao.
Ametoa pongezi hizo leo Jumanne (Agosti 26, 2025) wakati
aliposhiriki katika maadhimisho ya kilele cha miaka 64 ya Jeshi la Magereza
Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji
Tanzania, Ukonga jijini Dar es Salaam.
“Ninatoa pongezi za dhati kwa jeshi la magereza kwa
mafanikio haya, huu ni mpango kazi wenu, na tumeona faida na vijana hawa
waliokuja hapa wameeleza namna ambavyo wamenufaika na kazi hizi.”
Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne
Sagini amelipongeza Jeshi la Magereza kwa wepesi katika kutafsiri na kutekeleza
maelekezo ya Serikali na Viongozi mbalimbali na mengine bila kuwezeshwa fedha
kutoka Serikalini.
Amesema, Jeshi hilo limeendelea kufanyia kazi mapendekezo
yaliyotolewa na Tume ya Mhe. Rais ya kuboresha Vyombo vya Haki Jinai ikiwemo
maboresho ya programu za urekebishaji wa wafungwa.
"Ujuzi wanaoupata wafungwa kutokana na mafunzo
wanayoyapata yana umuhimu mkubwa katika kuwawezesha kufanya shughuli halali za
kujikimu pale watakarudi kwenye jamii na hivyo kuwafanya kutorudia kutenda
makosa."
Awali, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah
Katungu amesema Jeshi hilo limefanikiwa kuandaa mitaala mipya 10 ikiwa ni hatua za kuboresha utoaji wa mafunzo stahiki
kwa watumishi.
Amesema, Mitaala hiyo
imeandaliwa kwa kushirikiana na Chuo cha
Ustawi wa Jamii, Baraza la Taifa la
Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi. (NACTVET), Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW).
"Tumeandaa Mwongozo wa Program za Urekebishaji kwa Wafungwa. Mwongozo huu umeweka misingi thabiti na utaratibu wa Mapokezi, Tathmini, Urekebishaji na kuwaandaa wafungwa kurejea kwenye jamii wakiwa raia wema."
0 Maoni