Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana Mustafa,
amesema kuwa utambulisho wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) ni hatua
muhimu inayochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la
kurahisisha utoaji wa huduma za afya na kupunguza vifo na magonjwa ya kina mama
na watoto kwa wananchi wa Zanzibar.
Mkuu huyo wa Mkoa ameyasema hayo katika hafla ya utambulisho
na makabidhiano ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya
Zanzibar kwenda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, iliyofanyika katika
Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil, Kikwajuni Zanzibar.
Amesema kuwa wahudumu hao ni nguzo muhimu katika mapambano
dhidi ya maradhi mbalimbali na kuimarisha afya ya mama na mtoto. Aidha,
ameeleza kuwa dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ni kuwapandisha hadhi wahudumu hao kutoka kujitolea
(CHV) hadi kuwa wafanyakazi rasmi, ili wawe sehemu ya juhudi za Serikali katika
kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kuanzia ngazi ya jamii hadi
hospitali za rufaa.
Amewahimiza Wahudumu hao kufanya kazi kwa weledi, uadilifu
na bidii, wakishirikiana na viongozi wa serikali za mitaa na mikoa ili
kufanikisha azma ya Serikali ya kuimarisha afya ya jamii. Pia amewataka kuwa
waadilifu katika utendaji wao na kuwa tayari kushirikiana kwa karibu na
wananchi kwa lengo la kujenga jamii yenye afya bora.
Viongozi wa Wizara ya Afya wamepongezwa kwa mchango wao
katika kuwaendeleza wahudumu hao na kusimamia mchakato wa kuwatambua rasmi na
kuwakabidhi kwa viongozi wa mkoa na serikali za mitaa, hatua itakayochochea
maendeleo ya huduma za afya nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan
Khamis Hafidh, amesema nchi nyingi zilizoendelea zimefanikiwa katika huduma za
afya kupitia mfumo wa kinga unaotegemea wahudumu wa afya wa ngazi ya jamii.
Hivyo ni wakati muafaka kwa CHW kubeba jukumu hilo kama nguzo ya kwanza ya
uimarishaji wa huduma bora za afya kwa jamii.
Ameeleza kuwa jukumu jingine la CHW ni kuimarisha uelewa wa
afya katika jamii kwa kila kaya, shehia na wilaya, sambamba na kutoa elimu ya
kinga pamoja na uchunguzi wa awali na rufaa pale inapohitajika.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Amour
Suleiman Mohammed, amesema mpango wa kuwatambua CHW ni utekelezaji wa ahadi ya
Rais Dkt. Mwinyi. Hadi sasa jumla ya CHW 651 katika Mkoa wa Mjini Magharibi
wamehitimu mafunzo ya miezi sita na tayari wameanza kazi za kijamii.
Amefafanua kuwa CHW sasa watakuwa chini ya usimamizi wa
viongozi wa mikoa na wilaya, wakijikita zaidi katika kutoa elimu ya afya,
kushiriki katika kampeni za jamii, kupinga ukatili wa kijinsia, kushiriki
tafiti za afya na kusaidia kupunguza vifo na kuimarisha utoaji wa huduma bora
za afya.
Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar, Dkt. Salim
Slim, amesema uwepo wa CHW katika jamii ni nyenzo muhimu ya kusaidia Serikali
kupunguza rufaa zisizo za lazima kwa wagonjwa kwenda hospitali kubwa kwa kuwa
huduma za kinga zitapatikana mapema. Ameahidi kuwa Wizara itaendelea
kushirikiana nao ili kufanikisha malengo ya sekta ya afya.
Mratibu wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Halima Ali Khamis,
amesema hadi sasa jumla ya CHW 1,242 wamekamilisha mafunzo yao, huku wengine
1,054 wakiendelea na mafunzo, ikiwa ni sehemu ya uimarishaji wa upatikanaji wa
huduma za afya kwa wananchi katika maeneo yao.
Wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa ya WILLOSA na
D-Tree, Abdul-Wahid Habib na Anna Mikidadi, wamesema CHW ni kiunganishi muhimu
kati ya familia na vituo vya afya. Wamehimiza ushirikiano baina ya serikali na
wadau wengine katika kuhakikisha huduma bora za afya ya mama na mtoto
zinaimarika, huku wakiahidi kuendeleza matunda ya kazi chanya kwa jamii.
Kwa sasa, Mkoa wa Mjini Magharibi una jumla ya CHW 651
waliomaliza mafunzo na tayari wameanza kazi. Katika Wilaya ya Mjini, CHW 201
wamehitimu na kuanza kazi ambapo idadi kamili itakapokamilika itafikia 404.
Wilaya ya Magharibi “A” ina CHW 239 waliomaliza mafunzo, na idadi hiyo
ikikamilika itafikia 549. Wilaya ya Magharibi “B” ina CHW 211 waliomaliza
mafunzo na kuanza kazi rasmi; na idadi kamili itafikia 634 baada ya mafunzo
kukamilika.
Makabidhiano haya yaliambatana na kiapo cha utendaji kazi kilichotolewa kwa CHW na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh.
0 Maoni