Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kwa kushirikiana na taasisi
kutoka ndani na nje ya nchi, wameanza mchakato wa kuimarisha uzalishaji wa
mbegu bora za miti ili kukuza misitu ya viwanda na kuhifadhi mazingira.
Hayo yamejiri jana Agosti 6, 2025 katika Shamba la Miti Sao Hill, Wilaya
ya Mufindi mkoani Iringa, wakati wa ziara ya pamoja kati ya Kurugenzi ya Mbegu
ya TFS na washirika wake wa kimataifa wakiwemo FORLAND Tanzania, TAPIO kutoka
Finland na Chama cha Wahitimu wa Sayansi ya Misitu Tanzania (TTGAU).
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhifadhi Mkuu wa TFS, Dkt. Fortunate
Senya, alisema lengo kuu ni kuhakikisha mbegu bora za miti kama mikaratusi na
misindano zinazalishwa kwa viwango vya kitaifa na kimataifa, kwa ajili ya
kuhudumia mashamba ya miti ya viwanda na kuleta tija kiuchumi na kimazingira.
“Tumejionea namna miche ya miti iliyoboreshwa inavyokuza kwa ufanisi
katika bustani ya miche ya Irundi. Hii ni hatua muhimu kuelekea uhakika wa
mbegu bora, hasa kwa mashamba yanayohitaji kurejeshwa baada ya kuvunwa,”
alisema Dkt. Senya.
Katika ziara hiyo, timu ilitembelea pia Tarafa ya Pili ya Shamba Ihefu,
ambapo walikagua shamba maalum la kuzalisha mbegu za mikaratusi.
Wataalamu walibainisha mafanikio pamoja na changamoto zinazojitokeza,
huku wakisisitiza haja ya kuweka mikakati madhubuti kabla ya kuanzishwa kwa
mashamba mengine mapya ya uzalishaji wa mbegu.
Aidha, wadau hao walionesha kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na TFS
katika kulinda mashamba dhidi ya majanga ya moto hasa wakati wa kiangazi, jambo
walilolieleza kuwa ni sehemu muhimu ya usimamizi endelevu wa misitu.
Kwa mujibu wa TFS, Shamba la Miti Sao Hill ni miongoni mwa mashamba
yanayonufaika na mbegu bora zinazozalishwa na vituo vya taasisi hiyo kupitia
ushirikiano wa kimkakati na wadau wa uhifadhi. Mbegu hizo hutumika pia
kupunguza utegemezi wa misitu ya asili na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi.
Kwa upande wao, wawakilishi wa TAPIO Finland na FORLAND wamesema Tanzania
ina fursa kubwa ya kuwa kinara katika uzalishaji wa mbegu bora barani Afrika,
endapo utawekwa mkazo katika utafiti, teknolojia na usimamizi shirikishi.
0 Maoni