Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, leo
Agosti 22, 2025, amekutana na kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Mambo ya
Nje wa Sweden, Mhe. Maria Malmer Stenergard, katika ofisi za wizara hiyo jijini
Stockholm, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa
hayo mawili.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Matinyi aliwasilisha
salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, ambaye alimtaja kama Mwanadiplomasia namba moja wa taifa, huku
akisisitiza dhamira ya Tanzania kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kukuza
ushirikiano wa kiuchumi na Sweden.
Balozi Matinyi alieleza kuwa Tanzania imeendelea kuweka
kipaumbele kwenye ushirikiano wa kimataifa, hasa katika sekta za nishati,
elimu, afya, utafiti, mazingira, viwanda na miundombinu ikiwemo ujenzi wa Reli
ya Kisasa (SGR).
“Tanzania inatambua mchango mkubwa wa Sweden katika kusaidia
maendeleo ya sekta mbalimbali na tunaamini ushirikiano huu utaendelea kuleta
manufaa kwa pande zote mbili,” alisema Mhe. Matinyi.
Aidha, alibainisha kuwa hadi sasa jumla ya kampuni 101
kutoka Sweden zimewekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali, kwa thamani
ya zaidi ya dola za Marekani milioni 313.04, huku zikiwa zimezalisha ajira
takribani 3,877. Alisisitiza kuwa Tanzania inakaribisha kwa mikono miwili
wawekezaji kutoka Sweden ili kuendeleza biashara na miradi ya pamoja.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Mhe.
Stenergard, alieleza kuwa Sweden inaendelea kuthamini ushirikiano wake na
Tanzania, na iko tayari kupanua wigo wa mahusiano hayo, hasa kwenye biashara na
uwekezaji.
Vilevile, Waziri Stenergard alitoa pongezi kwa Tanzania kwa
mchango wake katika kulinda amani na usalama wa kimataifa, huku akihimiza
ushiriki wa Tanzania katika kutafuta suluhisho la kudumu la mgogoro kati ya
Ukraine na Urusi.
Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia zinazolenga kuimarisha nafasi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa, pamoja na kuhamasisha uwekezaji unaolenga maendeleo endelevu.
0 Maoni