Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari wa
Wanyamapori kutoka Mpanga Kipengele, chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA), linamshikilia Frank Alon (49), mkazi wa Uyole -
Nsalaga jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali bila kibali
halali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mbeya Benjamin Kuzaga, amesema Alon alikamatwa Agosti 17, 2025 majira ya saa
9:00 alasiri katika Kijiji cha Nsonyanga, Kata ya Mahongole, Tarafa ya Ilongo,
Wilaya ya Mbarali, wakati wa oparesheni za pamoja za misako na doria
zinazofanywa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na TAWA.
Taarifa hiyo imeelezwa kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na
meno manane (08) ya tembo yenye uzito wa kilo 31.6, ambayo alikuwa
akiyasafirisha kwa kutumia pikipiki aina ya TVS yenye namba za usajili MC 165 DDF.
Alidaiwa kuwa katika harakati za kutafuta mteja wakati aliponaswa na askari.
“Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa mtuhumiwa huyu ni mwindaji haramu ambaye amekuwa akijihusisha na ujangili katika hifadhi za taifa,” alisema Kamanda Kuzaga.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya likishirikiana
na Maafisa kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Tawi la Mbeya,
linamshikilia Ikupa Mwakibibi (32), mfanyabiashara na mkazi wa Mtaa wa Sae,
Kata ya Ilomba jijini Mbeya kwa tuhuma za kujiunganishia umeme kinyume cha
utaratibu wa shirika hilo.
Kamanda wa Polisi Kuzaga alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa
Agosti 18, 2025 saa 9:30 alasiri wakati wa oparesheni ya pamoja iliyofanyika
eneo la Sae, ambapo baada ya upekuzi nyumbani kwake, alikutwa akiwa na vifaa
mbalimbali mali ya TANESCO.
“Vitu vilivyokutwa ni pamoja na mita 19 za umeme, rimoti 45
na wayarola 25. Vyote hivyo ni mali ya TANESCO na vinatumiwa kwenye shughuli za
usambazaji wa umeme,” alisema Kamanda Kuzaga.
Jeshi la Polisi limesema uchunguzi zaidi unaendelea kuhusu matukio haya na mara taratibu zitakapokamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
0 Maoni