Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amekagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400
kutoka Chalinze hadi Zuzu Dodoma na
kueleza kutoridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo ambao ulipaswa kuwa umefikia asilimia 31 lakini kwa
sasa umefikia asilimia 24 tangu
kuzinduliwa kwake Novemba mwaka 2024.
Hali ya kusuasua kwa mradi imebainika wakati Dkt. Biteko
akikagua mradi huo katika Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino mkoani Dodoma
tarehe 20 Agosti 2025 ambapo Dkt. Biteko amemuagiza mkandarasi kampuni ya TBEA
ya China kuhakikisha kuwa anafidia muda wa kazi uliopotezwa wa asilimia Saba
ili mradi ukamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini.
Mwezi Novemba, 2024 Serikali ilikubaliana na mkandarasi kuwa
mradi huo ufanyike ndani ya miezi 19 tu badala ya miezi 22 kwani wakati mradi
unazinduliwa tayari kazi kubwa za awali zilikuwa zimeshafanyika ikiwemo za
upembuzi yakinifu na utoaji wa maeneo.
“ Leo ni miezi saba imepita tangu tuzindue mradi sawa na
asilimia 32 ya muda wote tuliokuwa tunahitaji
kutekeleza mradi huu, na tulitegemea mradi kwa sasa ufikie asilimia 31
lakini katika hali ya kushangaza mradi umefikia asilimia 24 tu jambo ambalo
halikubaliki,” amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko ameeleza kuwa, sababu zilizotolewa na Mkandarasi
za kuchelewesha mradi ikiwemo ya wananchi kugoma kutoa maeneo kwa madai ya
fidia na kukutana na miamba katika mkuza wa mradi hazikubaliki kwani wananchi
hao wana haki na lazima walipwe
fidia.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) kutumia mapato yake ya ndani
kulipa fidia wananchi waliopisha mradi.
Dkt. Biteko ametanabaisha kuwa mkandarasi alishaagizwa
asiutekeleze mradi huo kwa mazoea kutokana na umuhimu wake kwani kwa sasa miundombinu inayosafirisha umeme kwenda Dodoma kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP)
kupitia kituo cha Chalinze inabeba umeme kidogo kwa takriban megawati
240 tu ambayo ni sawa na mashine moja tu kati ya mashine 9 za JNHPP hivyo njia
hiyo mpya ya umeme ya kV 400 inayojengwa ni muhimu.
Amesisitiza kuwa njia mpya ya umeme ya kV 400 ni muhimu
kwani katika Mkoa wa Dodoma mahitaji ya umeme yanaongezka kila siku huku mkoa
huo pia ukiwa ni kitovu cha usambazaji umeme katika mikoa yote ya Magharibi
ikiwemo Singida, Tabora, Shinyanga Mara na Kigoma ambayo inategemea utulivu wa
umeme katika Mkoa wa huo na kwamba Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaagiza kuwa mradi huo usichezewe hivyo Mkandarasi
ahakikishe kuwa anaupa umakini mkubwa.
Kutokana na mradi huo kuwa nyuma katika utekelezaji, Dkt. Biteko
amemuagiza Mkandarasi kuja na mpango mpya wa utekelezaji wa kazi ukiwemo
wa kufidia muda uliopotezwa ambapo ametoa siku nne mpango wa fidia ya muda
uwasilishwe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati.
Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza mkandarasi kuongeza nguvu
kazi ya watu ili minara 917 ya umeme inayopaswa kujengwa kwenye mradi huo
ijengwe kwani kwa sasa mkandarasi amechimba takriban mashimo 100 tu kwa ajili ya usimikaji wa
minara. Pia amemtaka Mhandisi mshauri wa mradi kuhakikisha anasimamia mradi huo
kwa ufanisi na aeleze ukweli pale anapoona kuwa hauendi sawa.
Aidha amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,
kutengeneza timu itakayoungana na TANESCO kuusimamia mradi huo na kila wiki
taarifa itolewe kuwa umefikia wapi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa Wananchi
kutozuia utekelezaji wa miradi pale inapopita kwenye maeneo yao na Serikali kwa
upande wake itahakikisha kuwa wanapata haki wanazostahili kwani Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan ameshaelekeza kuwa hataki wananchi wafanyiwe dhuluma ambapo
wasaidizi wake wanahakikisha kuwa agizo hilo linatekelezwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mradi huo wa usafirishaji umeme wa kV 400
kunaenda kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha usambazaji umeme nchini.
Aidha, ameahidi kuyasimamia maelekezo yote yaliyotolewa na
Dkt. Biteko ya kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwezesha
umeme huo utakaofikishwa Dodoma, kusambazwa pia kwenye maeneo mengine nchini.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mtendaji
wa TANESCO, Lazaro Twange amesema Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo
wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma unakusudia kusafirisha umeme wote
unaozalishwa kutoka katika Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere
(Megawati 2,115) na kuingiza kwenye
gridi ya Taifa kisha kuufikisha kwenye
maeneo yote yenye mahitaji ya umeme.
Amesema mkataba na mkandarasi kampuni ya TBEA ulisainiwa
mwaka 2024 na mradi kuanza kutekelezwa mwezi Novemba 2024 ambapo mkandarasi
ameshalipwa awamu ya kwanza ya malipo ambayo ni shilingi za kitanzania bilioni
107 na mhandisi mshauri ameshalipwa asilimia 15 ya malipo yake.
Ameeleza kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu
na Waziri wa Nishati yatafanyiwa kazi
ikiwemo ya kuhakikisha kuwa mradi unakamilika mwezi Juni au kabla ya Juni 2026
kwa mujibu wa mkataba.
Aidha, Ameishukuru Serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 513 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo
ambao utakuwa na urefu wa kilometa 345 na kuhusisha minara ya umeme ipatayo 917
kutoka Chalinze mkoani Pwani hadi Zuzu mkoani Dodoma.
0 Maoni