Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa
utekelezaji wa Mradi wa Dhahabu wa Nyanzaga, unaotekelezwa kwa ubia kati ya
Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Perseus Mining Limited kupitia Kampuni ya
Nyanzaga Mining Company Ltd, utakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa
taifa na ustawi wa wananchi katika kipindi chote cha utekelezaji wake.
Amesema hayo leo Agosti 20, 2024 katika Kijiji cha Sotta
Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza akiwa Mgeni Rasmi katika Hafla ya Utiaji Saini Makubaliano ya
Nyongeza Kati ya Serikali na Kampuni ya Nyanzaga Mining Company Limited kwa
Ajili ya Uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Dhahabu Kupitia Kampuni ya Ubia ya Sotta
Mining Corporation Limited.
Katika Hafla hiyo, Serikali imesaini mkataba wa nyongeza na
Kampuni ya Nyanzaga Mining Limited kutoka asilimia 16 hadi 20 za umiliki wa
hisa za Kampuni ya Ubia ya Sotta.
Akizungumza katika Hafla hiyo, Waziri Mavunde amebainisha
kuwa zaidi ya shilingi trilioni 1 zinatarajiwa kuwekezwa katika utekelezaji wa
mradi huo, hatua ambayo itasaidia kufungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii
kwa Watanzania hususan wananchi wa Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza na taifa
kwa ujumla
Ameeleza manufaa ya Mradi huo kuwa ni pamoja na Ajira kwa
Watanzania kwani Mradi utatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja
kwa maelfu ya wananchi, na hivyo kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira;
Ushiriki wa Watanzania ambapo Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha
wananchi wanashiriki kikamilifu kupitia utoaji wa huduma na bidhaa mbalimbali
zinazohitajika kwenye mradi.
Mafanikio mengine ni Mapato ya Serikali kupitia kodi, tozo
na gawio la hisa za Serikali (20% free carried interest), ambapo mradi
utaiingizia Serikali mapato makubwa ambayo yataelekezwa kwenye miradi ya
maendeleo; Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ambapo Kampuni hiyo italazimika
kushirikiana na jamii katika kuboresha huduma za kijamii kama shule, afya, maji
na miundombinu pamoja na kusaidia miradi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Wizara ya Madini
itasimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha wananchi na taifa
kwa ujumla wananufaika ipasavyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameeleza kuwa Kampuni
ya Sotta Mining imerudisha leseni yake Serikalini, na Wizara itahakikisha
leseni hizo zinagawiwa kwa wananchi wa Wilaya ya Sengerema huku akiitaka
Kampuni ya Sotta kuendelea kutoa msaada wa kiufundi kwa wachimbaji wadogo, na
kuagiza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupeleka mtambo maalum wa
kuchoronga (drilling rig) ili kusaidia wachimbaji wadogo kuongeza tija.
Waziri Mavunde ameihakikishia Kampuni ya Perseus kuwa
haitajutia uamuzi wake wa kuwekeza Tanzania, kwani taifa lina sera bora,
mazingira rafiki ya uwekezaji, na dhamira ya kuhakikisha sekta ya madini
inawanufaisha Watanzania wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Perseus Bi.
Lee-Anne de Bruin ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha mazungumzo
hayo na hatimaye kusainiwa mkataba huo wa nyongeza kati ya Serikali na Kampuni
yetu ambapo utaruhusu shughuli za uzalishaji kuanza pindi shughuli za ujenzi
zitakapokamilika mwanzoni mwa mwaka 2027.
“Mradi huu utaleta manufaa makubwa kwa taifa hili mara
mbaada ya kuanza uzalishaji. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa
kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia yaliyosaidia kurahisisha mchakato
wa uwekezaji huu mkubwa,” amesema Bi. Lee-Anne.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda ameeleza kuwa
kiasi cha fedha cha dola za Marekani milioni 500 zitakazotumika kujenga mradi
huo, zitasaidia kubadilisha Mkoa wa Mwanza, na kwamba kuanzishwa kwa mradi huo
utasaidia zaidi kuongeza mapato ya Serikali katika Mkoa huo.
Awali akizungumza, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu
ameeleza kuwa, Mgodi huo utaletea taifa maendeleo endelevu, ni moja ya miradi
mikubwa zaidi ya madini Tanzania na utaleta faida kubwa kwa taifa na kwamba
utaingizia Serikali shilingi bilioni 400 lakini pia mapato kupitia Kodi, gawio
na vitu vingine, lakini pia utaleta ajira,
“mradi huu utaimarisha uchumi wetu, katika kipindi cha mnyukano wa uchumi duniani, kilichotusaidia ni madini, ni bidhaa inayotuletea fedha nyingi sana za kigeni na kusaidia kuimarisha uchumi wetu,” amesisitiza Mchechu.
0 Maoni