Tanzania na Japan zimesaini Hati ya Makubaliano ya
ushirikiano (MoU) katika uendelezaji wa rasilimali watu katika sekta ya ujenzi.
Uwekaji saini wa MoU hiyo umefanywa na Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo
(Mb) na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii
(anayeshughulikia Miradi ya Kimataifa) wa Japan, Mheshimiwa Kenichi Ogasawara
jijini Yokohama pembezoni mwa Mkutano wa TICAD9 Agosti 20, 2025.
Kupitia makubaliano hayo na kwa kuzingatia teknolojia ya
Japan na kampuni zake katika miundombinu bora inayodumu kwa muda mrefu na
inayostahimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi, Tanzania itanufaika
kuwajengea uwezo vijana wa kada za uhandisi na ujenzi kupata teknolojia na
ujuzi wa Japan ili waweze kujiajiri katika kada za ujenzi na kupata ajira
katika kampuni za Japan.
Makubaliano hayo
yatasaidia katika kushirikisha vijana wa Tanzania na sekta binafsi katika
utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kupitia sekta ya miundombinu
bora ambayo ni sekta mtambuka katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika kuingia makubaliano hayo na Japan katika sekta ya ujenzi, Japan imewahi kuingia makubaliano haya na baadhi ya nchi za kusini mashariki mwa Asia ambazo kupitia teknolojia bobevu ya Japan katika miundombinu bora imechagiza maendeleo ya kiuchumi ya nchi hizo.
0 Maoni